BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
UONGOZI wa Simba leo umetangaza kumsimamisha beki wao Hassan Kessy ambaye atakosa mechi tano sawa na muda wa kumalizika kwa mkataba wake ambapo yeye ametamka kwamba bado anajihesabia ni mchezaji wao na kama wamevunja mkataba basi wamlipe chake.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa klabu hiyo Haji Manara ilieleza kuwa mechi tano alizopigwa marufuku beki huyo ni sawa na mwezi mmoja uliobaki kwenye mkataba wake hivyo tayari mchezaji huyo muda wake wa kukaa Simba utakuwa umekwisha.

Kessy amesimamishwa kwa kosa la kumchezea faulo mshambuliaji wa Toto Africans, Edward Christopher na hivyo kupewa kadi nyekundu na kuisababishia timu yake kucheza ikiwa pungufu ambapo Simba ilifungwa bao 1-0, mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kessy amepata taarifa hizo mara tu baada ya viongozi wake kutangaza na kusikitika kwamba yeye alifanyiwa kitendo kibaya na kipa wao Vincent Angban lakini hajachukuliwa hatua yoyote ila yeye aliyefanya kosa la kimchezo la bahati mbaya ameadhibiwa.

''Nimesikia taarifa hiyo na tayari  nimewasiliana na meneja wangu  (Athuman Tippo) ila bado najihesabia nipo kwenye mkataba na Simba, kama wao wamevunja mkataba wangu basi wanastahili kunilipa stahiki zangu, hizi ni changamoto japokuwa mimi nimefanyiwa jambo baya na wamekaa kimya.

''Mkataba wangu umebaki wa mwezi mmoja kwa maana unamalizika mwishoni mwa msimu huu. Daima nitaendelea kumshukuru na kumuomba Mungu kwa kila hatua ninayopitia, hivyo haya yote yanayotokea namwachia yeye,'' alisema Kessy.

Simba imebakiza mechi tano ambazo  ni ile ya Azam, Mwadui, Majimaji, Mtibwa Sugar na JKT Ruvu.

Post a Comment

 
Top