BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakar Kagoma, Chamazi

TIMU ya soka ya Azam Fc imebanwa mbavu na Ndanda Fc kwa kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kiporo wa ligi kuu ya Vodacom uliopigwa kwenye dimba la Azam Complex Chamazi.

Azam walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Ramadhan Singano 'Messi' katika dakika ya 10 akimalizia krosi ya Michael Balou kabla Didier Kavumbagu hajaipatia bao la pili dakika ya 42 hivyo kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao hayo mawili.

Kipindi cha pili Ndanda walionekana kubadilika na kuanza kutengeneza nafasi za mabao ambapo katika dakika ya 50 jitihada zao zilizaa matunda baada ya Atupele Green kuipatia bao kwa mkwaju wa penati uliotokana na Paul Ngalema kufanyiwa madhambi na kipa wa Azam Aishi Manula ndani ya eneo la hatari.

Baada ya bao hilo Ndanda walicharuka zaidi na kama si kukosa umakini kwa wachezaji wake Omar Mponda na Salum Minely basi wangeweza kupata mabao mengine katika dakika za 55 na 68.

Katika dakika ya 86, Ndanda walijihakikishia kuondoka na pointi moja baada ya beki wa Azam Aggrey Moris kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na Ahmad Msumi aliyeingia kuchukua nafasi ya Minely.

Mabadiliko mengine kwa upande wa Ndanda ni Burhan Rashid aliyeingia badala ya Masoud Ally huku Azam wao wakiwatoa Racine Diof, Waziri Salum na Kavumbagu na nafasi zao zikichukuliwa na Mudathir Yahaya, David Mwantika na John Bocco.

Diof na Pascal Wawa ndio wachezaji pekee waliozawadiwa kadi za njano katika mchezo huo ambao matokeo yake ya sare yameifanya Azam ifikishe pointi 52 baada ya kushuka dimbani mara 23 wakibakia katika nafasi yao ya tatu nyuma ya Simba (57) na Yanga (53).

Katika mchezo mwingine wa Ligi kuu ya Vodacom, Majimaji ya mjini Songea imetandika Coastal Union mabao 2-0 yaliyofungwa na Danny Mrwanda pamoja na Lucas Kikoti.

Post a Comment

 
Top