BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
KLABU ya Yanga imeitikia wito wa kufanya uchaguzi na imemteua Salum Mapande kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ambaye atapendekeza tarehe ya kufanya uchaguzi huo.

Awali klabu hiyo ilimteuwa Wakili Alex Mgongolwa lakini baadaye aliomba kuachia nafasi hiyo kutokana na matatizo ya kifamilia na uteuzi wa Mapande umekuja baada ya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuweka msisitizo wa uchaguzi huo.

Hivi karibuni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye alitoa agizo kwa Yanga kufanya uchaguzi ndani ya siku saba na kuitaka BMT kusimamia zoezi hilo na kuhakikisha Yanga wanafanya uchaguzi wao.

Yanga sasa inaongozwa na kamati ya muda chini ya Mwenyekiti, Yusuph Manji ambaye bado hajaweka wazi nia ya kugombea tena nafasi hiyo ambapo muda wake ulimalizika tangu mwaka jana.

Msemaji wa klabu hiyo, Jerry Muro alithibitisha hilo na kusema kwamba Mapande ndiye atakayeunda kamati yake atakayosaidiana nayo kwenye uchaguzi.

"Klabu inamsikiliza Mapande ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti, yeye ndiye mwenye mamlaka yote kwasasa kwamba lini fomu zianze kutolewa, tarehe ya uchaguzi, muda wa kufanya kampeni na mambo mengine yanayofanywa katika kipindi hicho.

"Ni lazima uchaguzi ufanyike na tumewaambia BMT chini ya Katibu, Mohammed Kiganja maana taarifa tuliyopewa ni kama kutukumbusha tu. Kwa kawaida uchaguzi unatakiwa kutolewa tamko kwa siku 60 nadhani Mapande anaelewa zaidi mchakato mzima," alisema Muro.

Habari za ndani kutoka Yanga zinaeleza kuwa pamoja na kuteuwa Mwenyekiti huyo lakini huenda ikawa ngumu kwa klabu hiyo kufanya uchaguzi kwa kipindi ambacho wamepewa kwani wanapambana kuhakikisha wanatetea ubingwa hivyo hawataweza kuingiza kati suala la uchaguzi.

Imeelezwa kuwa uchaguzi huo utafanyika mara baada ya ligi kumalizika mwezi ujao, Yanga pia inashiriki michuano ya Mabingwa wa Afrika ambapo keshokutwa Jumapili wataifuata Al Ahly nchini Misri kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ambapo mechi ya awali iliyochezwa Uwanja wa Taifa timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1.

Post a Comment

 
Top