BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
ZIMEBAKI siku 22 tu ligi kuu Tanzania bara inayodhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi, Vodacom ifikie tamati na bingwa ambaye ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika atavalishwa taji Mei 21.

Mengi yametokea katika michuano hiyo ambayo bingwa mtetezi, Yanga inaongoza ligi ikiwa imeshajikusanyia pointi 62 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 58 huku wekundu wa Msimbazi Simba wakishika nafasi ya tatu kwa pointi zao 57.

Yafuatayo ni mambo matano ya kustaajabisha yaliyotokea kwenye ligi hiyo hadi leo hii ambapo baadhi ya timu zimebakiza mechi tatu tu zimalize kazi.

1. Kiiza azifunika Kagera, Coastal na African Sports
African Sports ndio timu iliyofunga mabao machache zaidi (11) kwenye msimamo wa ligi kuu huku Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' wenyewe wakiwa wametupia mabao 15 tu katika michezo 27 waliyocheza.


Timu nyingine ambayo ina mabao machache ni Kagera Sugar ambayo imefunga 18 pekee, cha kustaajabisha ni kwamba, straika wa Simba, Hamis Kiiza peke yake ameshatingisha nyavu za timu pinzani mara 19 akizizidi timu hizo tatu ambazo zipo mkiani mwa ligi hiyo.

2. Yanga haijapoteza mchezo wowote Taifa
Ukisikia matumizi bora ya uwanja wa nyumbani basi ndio haya.... Watoto wa Jangwani, Yanga hadi sasa wameshacheza mechi 15 katika dimba la taifa. Habari ni kwamba mashabiki wa timu hiyo ambayo ndio wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa kwa sasa, hawajawahi kutoka katika uwanja huo wakiwa vichwa chini tangu mchezo wao wa kwanza Septemba 13, 2015

Katika mechi hizo 15, Yanga wamejizolea pointi 43 baada ya kuzifunga timu 14 na kutoka sare (1-1) mechi moja ambayo walipepetana na wauza 'Ice cream' wa Chamazi, Azam. 


Timu ambazo zilifungwa na Yanga katika uwanja huo ni pamoja na Coastal Union (2-0), Prisons (3-0), JKT Ruvu (4-1), Toto Africans (4-1), Stand United (4-0), Mbeya City (3-0) na Ndanda Fc (1-0).

Zingine ni Majimaji (5-0), Simba(2-0), African Sports (5-0), Kagera Sugar (3-1), Mwadui Fc (2-1), Mtibwa Sugar (1-0) na Mgambo JKT (2-1)

3. Simba yaachana na 'Ufundi wa Makabati'
Msimu uliopita Simba ilishindwa kupata ubingwa kutokana na kuathiriwa na idadi kubwa ya sare walizopata. Hali ya kutoka sare michezo mingi iliwanyima raha wapenzi na wanachama wa timu hiyo hasa pale watani zao Yanga walipowabatiza jina na kuwaita 'Wazee wa Makabati'.


Mambo yamekuwa tofauti sana msimu huu ambapo wekundu hao wa Msimbazi ndio timu ambayo imetoka sare michezo michache zaidi. Wakati Ndanda wakipata sare 12, Prison 11 na Toto tisa, Simba wao wamepata sare tatu pekee.

Simba ambayo bado ina nafasi ya kutwaa ubingwa msimu huu, ilitoka droo na Mwadui (1-1), Azam (2-2) na Toto (1-1).

4. Mzawa mmoja tu tano bora ya wafungaji
Timu za Yanga, Simba na Azam zimekuwa zikiongoza kwa kusajili wachezaji toka nje ya mipaka ya Tanzania, mwanzoni ilionekana kama 'fasheni' tu lakini ni dhahiri kuwa wachezaji hao wamekuwa wa msaada mkubwa katika timu hizo.

Namba hazidanganyi, ukitazama majina matano ya kwanza katika orodha ya wafungaji bora utafanikiwa kuliona jina la mtanzania mmoja tu, Elius Maguri wa Mwadui ambaye licha ya kukaa benchi katika michezo mingi, amefanikiwa kutupia mara 11 huku aking'ang'ana katika nafasi ya nne.


Wachezaji wa kigeni waliopo kwenye orodha hiyo ni Kiiza (19), Amissi Tambwe (18), Donald Ngoma (14) na Kipre Tchetche (10)

5. 'Collabo' ya timu za Tanga haifui dafu kwa Yanga
Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 62 huku ikiwa imefunga mabao 59 ambayo hata ukichanganya mabao yote yaliyofungwa na timu za Tanga kwa maana ya Mgambo (21), Sports (11) na  Coastal (15) bado hayayafikii yale ya Yanga.

Jumla ya mabao ya timu hizo zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja ni 47 ambayo ni mabao 12 pungufu ya yaliyofungwa na wanajangwani hao.

Post a Comment

 
Top