BOIPLUS SPORTS BLOG

KIKOSI cha Real Madrid kinachonolewa na Zinedine Zidane leo kimeibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa ligi kuu nchini Hispania 'La Liga', mechi iliyochezwa katika dimba la Nou Camp jijini Barcelona.

Licha ya kosakosa kadhaa, timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa hazijafungana. Barca walifanya mashambulizi mengi zaidi lakini umakini wa walinzi wa Madrid walioongozwa na Sergio Ramos pamoja na Pepe ulizima majaribio yao.

Barca walikianza kipindi cha pili kwa kasi wakionekana wazi kuhitaji bao la kuongoza ambapo katika dakika ya 54 Lionel Messi alipiga shuti lililookolewa na kipa Kaylor Navas na kuwa kona ambayo ilimkuta Gerald Pique aliyeitumbukiza wavuni dakika ya 56 kwa kichwa.

Katika dakika ya 62 Karim Benzema aliisawazishia Madrid kwa tiktaka akimalizia krosi ya Toni Kroos ambayo ilimgonga kwanza mlinzi wa Barca.

Dakika chache baada ya Gareth Bale kukataliwa bao lake kwa madai kuwa alikuwa ameotea, Ramos aliondolewa uwanjani kwa kadi nyekundu katika dakika ya 83 hiyo ikiwa ni kadi yake ya pili ya njano baada ya kumfanyia madhambi Luis Suarez.

Wakati Ramos hajafika chumbani, Cristiano Ronaldo aliipatia Madrid bao la pili akimalizia krosi ya Bale hivyo kuwafanya weupe hao wa Santiago Bernabeu waibuke na pointi zote tatu katika dimba la Nou Camp.

Kwa ushindi huo Madrid wamefikisha pointi 69 huku Barca wakisalia na pointi zao 76 katika nafasi ya kwanza. Atletico Madrid wao wamebakia nafasi ya pili kwa pointi 70 baada ya kuifunga Real Betis mabao 5-1 mqpema jioni ya leo.

Video za mabao yote ya mechi hii zinapatika kwenye ukurasa wetu wa Facebook: Boiplus Blogspot na ule wa Instagram @boiplus_blogspot

Post a Comment

 
Top