BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
BEKI wa kulia wa klabu ya Azam Shomari Kapombe amegundulika kuwa na tatizo kwenye mzunguko wa damu na  sasa atakosa michezo yote iliyobaki ya ligi kuu pamoja na ile ya kombe la shirikisho.

Kapombe ambaye aliondoka nchini Alhamisi iliyopita kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake na kukosa mechi ya kombe la shirikisho dhidi ya  Esparance iliyochezwa jana, sasa atakaa nje ya uwanja hadi mwishoni mwa msimu huu.

Daktari wa timu hiyo Juma Mwimbe ameithibitisha BOIPLUS kukosekana kwa mchezaji huyo kiraka mwenye uwezo wa kucheza namba nyingi uwanjani na uwezo mkubwa wa kukaba na kupandisha mashambukizi hasa akitokea upande wa kulia.

"Ni kweli kabisa Kapombe atakosa michezo yote iliyosalia msimu huu baada ya ugonjwa alionao kuhitaji muda mrefu ili kuwa fiti na mechi zikiwa zimebaki saba kumalizika kwa ligi," alisema Mwimbe.

Kapombe alipata tatizo hilo akiwa nchini Chad alipokuwa akiitumikia timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' na kupata ushindi wa goli 1-0 na ndipo uongozi wa Azam ukaamua kumpeleka Afrika Kusini kwa uchunguzi zaidi.

Kiraka huyo ndiye kinara wa magoli kwa upande wa mabeki baada ya kufunga magoli nane huku akishika nafasi ya tatu kwa ufungaji kwenye timu hiyo nyuma ya John Bocco mwenye magoli kumi na Kipre Tchetche mwenye magoli tisa.

Kapombe atakaa nchini Afrika Kusini kwa mwezi mmoja ili kuendelea kupata matibabu kabla ya kurejea nyumbani.

BOIPLUS inamtakia Kapombe nafuu ya mapema ili arudi katika majukumu yake

Post a Comment

 
Top