BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
KIUNGO wa Mbeya City, Medson Mwakatundu amerejea kwenye timu yake hiyo baada ya timu ya Geita Gold Soprts kushindwa kupanda daraja kutokana na kutuhumiwa kujihusisha na upangaji wa matokeo kwenye mechi ya mwisho ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Kiungo huyo tayari yupo kwenye kambi ya City inayojiandaa na mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa April 30, Uwanja wa Manungu, Turiani ikisaka pointi za kuwabakiza kwenye ligi ingawa ina nafasi ya kubaki kwa ajili ya msimu ujao.

Mwakatundu alijiunga na Geita mapema mwaka huu kwa mkopo baada ya kukosa nafasi ya kucheza na hivyo viongozi wa City waliamua wamepeleka huko ili kulinda kiwango chake. Katika mechi ya hiyo ya mwisho Geita iliifunga Kanembwa JKT bao 8-0 wakati Polisi Tabora ambayo pia ilishushwa daraja iliifunga JKT oljoro bao 7-0.

Katibu Mkuu wa City, Emmanuel Kimbe amethibitisha kurudi kwa kiungo huyo aliyekuwa akiichezea timu yao ya vijana: "Tulimpeleka huko kupata uzoefu maana huku kwetu alikuwa hapati nafasi ya kucheza japokuwa tulimpandisha kwenye timu ya wakubwa, amerudi kwasababu ana mkataba na Mbeya City, tunaamini atafanya vizuri kwani amepata uzoefu kwa kucheza mechi nyingi," alisema Kimbe.

Kwa upande wa Mwakatundu alisema: “Nimecheza mechi zote za FDL na pia mechi mbili za Kombe la FA, nashukuru Mungu nimerudi sasa naweka akili yangu kwenye timu yangu, nawashukuru viongozi na mashabiki wa timu ya Geita kwa ushirikiano wao, hakika wamefanya kila jema kwangu na nimejifunza mengi kutoka kwao, kazi yangu ilikuwa ni kucheza hivyo juu ya uamuzi uliotolewa kwa Geita viongozi ndiyo wanajuwa.”

Post a Comment

 
Top