BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
NAHODHA msaidizi wa timu ya Simba Jonas Mkude amefunguka kuwa kipigo cha goli 1-0 walichokipata dhidi ya Toto African kimewaumiza sana wachezaji kwakuwa walitegemea kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Mkude aliyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi kuu kati ya Simba na Toto Africans ambapo kufungwa kwa Simba kumeifanya isalie na pointi zake 77 katika nafasi ya pili nyuma ya Yanga yenye pointi 79.

"Ligi inapoanza kila timu inakuwa na dhamira ya kuchukua ubingwa lakini matokeo uwanjani yanakuwa tofauti na matarajio ya wengi, tulijiandaa kwa ushindi katika mchezo huu lakini ndio hivyo tena tumepoteza."

Mkude pia amewasihi mashabiki wa timu hiyo kuacha kuwashutumu wachezaji kwa matokeo yanayopatikana kwani hata wao yanawaumiza na wanajitahidi kucheza vizuri lakini mwisho wa siku mambo yanakuwa si mazuri kwa upande wao.

"Hiki ni kipindi cha wana Simba wote kushikamana ili tuweze kufanya vizuri kwani bila sapoti toka kwao sisi wachezaji na viongozi pekee hatutaweza kumaliza vizuri ligi hii," alisema Mkude.

Simba imepoteza mechi mbili ndani ya wiki moja baada ya Jumatatu iliyopita  kutolewa kwenye michuano ya kombe la FA na Coastal Union kwa kufungwa magoli 2-1.

Simba inatakiwa ipambane kufa na kupona ichukue taji la ligi kuu Tanzania bara ili ipate nafasi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa barani Afrika ambayo hawajashiriki tangu msimu wa 2011/2012.

Post a Comment

 
Top