BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
NAHODHA Msaidizi wa timu ya Simba Jonas Mkude amewaomba radhi wapenzi na mashabiki wa timu hiyo baada ya kuondolewa kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la FA kwa kufungwa bao 2-1 dhidi ya Coastal Union.

Mkude alisema mashabiki wengi walitegemea ushindi kwa kuwa timu yao ipo kwenye kiwango bora kiuchezaji na pia walionesha kandanda safi lakini bahati ilikuwa upande wa Coastal ambao walipata nafasi chache na kutumia mbili ambazo zimewawezesha kutinga hatua ya nusu fainali.

"Mashabiki wetu hawakujisikia vizuri hata sisi wachezaji na benchi la ufundi lakini ndiyo imetokea inabidi tukubali  ni hali ya mchezo na tunaelekeza nguvu kwenye ligi," alisema Mkude.

Katika mchezo huo uliopigiwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba ilitawala muda mwingi na kutengeneza nafasi nyingi ili  walishindwa kuzitumia hasa kipindi cha kwanza huku golikipa chipukizi wa Wagosi wa Kaya, Fikirini Bakari akifanya kazi ya ziada kupangua michomo ya wachezaji wa Simba.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara,  Coastal Union wanaburuza mkia wakiwa na pointi 19 baada ya kucheza michezo 26 huku Simba wakiwa vinara baada ya kujikusanyia pointi 57 baada ya kushuka dimbani mara 24.

Coastal sasa imejiunga na Yanga, Azam na Mwadui katika hatua ya nusu fainali ya kombe la FA ambayo droo yake itafanyika leo usiku.

Post a Comment

 
Top