BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
MAANDALIZI hafifu ya mechi za kimataifa ndio sababu ya timu za Tanzania kushindwa kufanya vizuri na kuwa wasindikizaji kila mwaka.

Kauli hiyo imetolewa na mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa na klabu ya Simba Zamoyoni Mogela alipokuwa akizungumzia kutolewa kwa Yanga na Azam katika michuano ya kimataifa.

Timu ya Yanga ilikuwa inawakilisha nchi katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika na kutolewa na Al-Ahly ya Misri huku Azam iliyokuwa ikishiriki kombe la shirikisho ilitupwa nje na Esparance ya Tunisia.

Mshambuliaji huyo ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa stars kilichoiwakilisha nchi kwenye michuano ya kombe la mataifa barani Afrika 1980 alisema ili kufanya vizuri katika michuano hiyo lazima kuwe na maandalizi makubwa kuanzia viongozi, benchi la ufundi na wachezaji.

"Wachezaji wanatakiwa waandaliwe kimwili na kiakili kulingana na ukubwa wa mechi ili kuepuka kadi zisizo za lazima ambazo zinaigharimu timu," alisema Mogela.

Aidha Mogela alisema wachezaji wa siku hizi hawachezi kwa kujituma kama ilivyokuwa wakati wao huku wakilipwa mamilioni.

"Utakuta mchezaji anacheza mechi ya ligi kama vile anacheza bonanza na ukiangalia analipwa mshahara mkubwa amepangishiwa nyumba na ana gari la kutembelea," alisema Mogela.

Yanga na Azam zimetua jijini Dar es Salaam mchana wa leo na zote mbili zimeingia kambini kujiandaa na mechi zao za nusu fainali ya kombe la FA dhidi ya Coastal Union na Mwadui. 

Post a Comment

 
Top