BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma na Akram Msangi, Dar
KIUNGO mshambuliaji kinda wa Coastal Union, Juma Mahadhi ameziita klabu za Simba na Yanga kukaa nae meza moja endapo watahitaji huduma yake msimu ujao.

Mahadhi ambaye anasifika kwa kuwa na kipaji cha hali ya juu ametokea kwenye timu ya vijana ya Coastal kabla ya kupandishwa kikosi cha wakubwa na kufanya vizuri huku kocha Ally Jangalu akimpa nafasi ya kuanza katika michezo mingi.

Tayari timu kadhaa zinazoshiriki ligi kuu  ya Vodacom zimeonesha nia ya kutaka kumsajili kiungo huyo huku yeye mwenyewe akiweka wazi kuwa timu itakayofikia makubaliano nae atajiunga nayo bila tatizo kwavile ligi ikiisha atakuwa huru.

"Mkataba wangu unaisha mwishoni mwa msimu na timu kadhaa zimenifuata lakini hakuna ambayo tumefikia makubaliano, ila naamini hadi ligi ikiisha kila kitu kitakuwa wazi," alisema Mahadhi.

Aidha kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20 ambaye iliifungia timu yake bao la ushindi ilipopambana na Yanga jijini Tanga kwenye mchezo wa ligi kuu, amejiwekea malengo ya kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania ifikapo mwaka 2018.

Juma ni mpwa wa kiungo wa zamani wa Yanga Waziri Mahadhi ' Mendieta' ambaye aling'ara sana na mabingwa hao mwanzoni mwaka miaka ya 2000.

Post a Comment

 
Top