BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
STRAIKA wa Yanga, Paul Nonga amekuwa akikumbana na ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho kutoka kwa mastraika wa kigeni, Amissi Tambwe na Donald Ngoma lakini uongozi wake wa zamani wa Mwadui FC wamemfungulia milango kama atahitaji kurudi kwao.

Yanga ilimsajili Nonga akitokea Mwadui FC kwa mkataba wa miaka miwili lakini anashindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili  kuonyesha cheche zake ndani ya kikosi hicho kinachoshiriki michuano ya kimataifa ya Mabingwa wa Afrika.

Kulikuwepo na taarifa kwamba huenda Yanga msimu ujao wa Ligi Kuu wakamrudisha kwenye timu yake ya zamani kwa mkopo ikiwa ni lengo la kumsaidia kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ambapo Katibu Mkuu wa Mwadui FC, Ramadhan Kilao amesema milango kwa Nonga iko wazi.

"Hata alipokuwa anaondoka tulimwambia akijisikia kurudi kwetu ni  ruksa. Nonga bado ni mchezaji mzuri ila tatizo lipo kwenye ushindani wa namba.

"Kuna wachezaji wa kulipwa pale ambao si rahisi kuwakalisha benchi, hivyo kama itatokea Yanga wakaamua kumrudisha kwetu kwa mkopo sisi hatuna tatizo tutamkaribisha na kumpokea," alisema Kilao

Mwadui kwa sasa inajiandaa na mechi dhidi ya Yanga huku ikisubiri kupangiwa timu pinzani kwenye michuano ya Kombe la FA katika hatua ya nusu fainali ambapo timu tatu tayari zimetinga hatua hiyo ikiwemo Yanga na Azam.

Timu ya Simba na Coastal Union zinasubiri kucheza hatua ya robo fainali ili apatikane mshindi atakayetinga hatua ya nusu fainali kuungana na timu hizo.

Post a Comment

 
Top