BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
WACHEZAJI wawili wa Ndanda FC, Salvatory Ntebe na Kigi Makasi huenda wakakosa mechi yao ya kesho dhidi ya Mwadui FC ambayo itachezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara kutokana na kuwa majeruhi.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hamis Malale alisema kuwa bado wachezaji hao hawapo fiti lakini leo jioni atawaangalia kama wataweza kuingia uwanjani kesho vinginevyo hilo litakuwa pengo na pigo kwao.

Alisema kuwa hawapaswi kupoteza mechi zao zilizobaki hasa za nyumbani ambazo zitawasaidia kuwabeba ili wabaki na pointi zitakazowabakiza kwenye ligi msimu ujao, vinginevyo mambo yao yatakuwa magumu kama watapoteza mechi hiyo ya Mwadui na nyingine mbili zitakazochezwa uwanjani hapo.

"Hawa wote wapo kwenye kikosi cha kwanza, kama hawatakuwa fiti basi sitaweza kuwatumia ila nitawaangalia zaidi maendeleo yao leo jioni, ni pigo kwetu kwasababu kipindi hiki ni kigumu kwetu pointi tulizonazo hatuwezi kusema zinatosha kutubakiza kwenye ligi tunahitaji kupambana zaidi angalau tupate pointi sita nyumbani kati ya tisa kwenye mechi tatu za hapa," alisema Malale.

Mpaka sasa Ndanda ina pointi 27 ambazo ni sawa na Mbeya City pamoja na Toto Africans huku ikiwa imecheza mechi 25 na inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.


Mechi nyingine za VPL zitakazochezwa kesho ni kati ya Mtibwa Sugar na Prisons wakati African Sports wataikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Post a Comment

 
Top