BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Azam FC, inashuka dimbani leo kuwavaa Esperance  ya Tunisia, katika mchezo wa raundi ya pili ya michuano hiyo utakaopigwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Azam ilikata tiketi ya raundi hiyo baada ya kuibomoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 7-3. Ilishinda mchezo wa kwanza mabao 3-0 na marudiano ikashinda bao 4-3.

Esperance ilifika raundi hiyo baada ya kuitoa Renaissance FC kutoka Chad kwa mabao 7-0. Mchezo wa kwanza ilishinda mabao 2-0 na ule wa marudiano wakaitandika mabao 5-0. Mshindi wa pambano hilo, atakata tiketi ya kuingia hatua ya makundi.

BOIPLUS inaelezea jinsi kikosi cha Azam kilivyo katika safu zake zote.

FOWADI HATARI, UKUTA LOH!
Katika michezo yake mitatu ya hivi karibuni ngome yake imeruhusu mabao sita. Kwenye mchezo wa marudiano na kombe la shirikisho dhidi ya Bidvest Wits waliruhusu magoli matatu na matatu mengine kwenye ligi wakifungwa bao moja katika sare ya 1-1 na Toto Afrika na mawili wakifungwa na Ndanda FC.
Kibaya zaidi katika magoli hayo sita matano yamefungwa kwenye Uwanja wao wa Chamazi.


Washambuliaji wake, Kipre Tchetche na John Boco pamoja na kiraka Shomari Kapombe wanajitahidi kupachika mabao kila wanapopata nafasi lakini mabeki wamekuwa wakiwaangusha kwa kuruhusu wapinzani wao kutikisa nyavu zao.

VIPORO KUSHUSHA MORALI 
Baada ya kufanikiwa kuwatoa Bidvest, Azam walicheza mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Prison na kushinda mabao  3-1 na tangu hapo hawakushinda tena zaidi ya kutoka sare mbili dhidi ya Toto Africans na Ndanda FC.

Wachambuzi wa masuala ya soka wanasema ni hatari kuelekea kwenye michezo ya kimataifa tena ukikutana na timu kubwa kama Esparence huku ukiwa hauna matokeo mazuri kwenye ligi ya nyumbani. Kuna uwezekano mkubwa kwa matokeo hayo kushusha morali ya wachezaji wa Azam kuelekea pambano hilo.

PIGO LA KAPOMBE
Hakuna ubishi kwa sasa Kapombe ndiye beki bora wa kulia ambaye ana uwezo mkubwa wa kukaba, kupiga krosi zenye madhara kwa timu pinzani, kupandisha timu kutokea pembeni na kufunga magoli.


Mchezaji huyo atakosekana baada ya kuugua mafua makali yaliyopelekea akimbizwe nchini Afrika ya kusini kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Mpaka sasa Kapombe amefunga mabao nane kwenye ligi na mawili kwenye Kombe la FA na uwezo mkubwa alionao wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani ambayo ingekuwa faida kubwa kwa Azam katika mchezo huo.

NI MUDA WA WAWA KUMPUMZISHWA
Baada ya kurejea kwa beki Aggrey Moris akitoka kupona majeraha ya goti ni muda sasa kwa benchi la ufundi la Azam kumpumzisha beki kisiki Paschal Wawa raia wa Ivory  Coast. 

Wawa ametumika kwa muda mrefu bila kupuzimka na yawezekana hii imemsababishia kuanza kufanya makosa ambayo yamekuwa yakiigharimu timu kutokana na uchovu ambao kwa lugha ya kitaalamu unaitwa 'fatique'.

AZAM IMESHAANZA KUPATA UZOEFU
Hii ni mara ya tatu kwa Azam kucheza michuano hiyo mikubwa Afrika. Ilishiriki mara ya kwanza Kombe la Shirikisho mwaka 2014 na kuishia raundi ya nne baada ya kutolewa na AS FAR ya Morocco kwa mabao 2-1.


Azam ilicheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliofuata na kutolewa na mabingwa wa Sudan, El Merreikh, raundi ya kwanza baada ya kuchapwa mabao 3-2. Mchezo wa marudiano ilitandikwa mabao 3-0.

UONGOZI WANENA
Mkurugenzi wa Azam FC, Saady Kawemba alisema kwa upande wa uongozi umekamilisha kila kitu kilichobaki ni wachezaji kutimiza wajibu wao huku akidai ushindi utapatikana hata kama itakuwa kwa ugumu lakini lazima upatikane.

BOIPLUS inawatakia kila la heri AZAM FC katika mchezo huo

Post a Comment

 
Top