BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
SHIRIKISHO la mpira wa miguu Tanzania TFF limetoa ratiba ya kombe la FA katika hatua ya nusu fainali itakayochezwa Aprili 24, droo iliyooneshwa moja kwa moja na kituo cha Azam TV.

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga imepangiwa kucheza na Coastal Union katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu hasa kutokana na historia ya timu hizo zinapokutana katika uwanja huo.

Mabingwa hao mara 25 wa ligi kuu Tanzania bara wameingia hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kuwatoa Ndanda FC ya Mtwara baada ya kuwachapa magoli 3-1 huku Coastal  wakiwatoa Simba kwa magoli 2-1.

Mechi nyingine ya nusu fainali itafanyika katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ambapo Mwadui FC itawakaribisha wauza 'Ice cream' wa jiji la Dar es Salaam, Azam FC ambayo licha ya kushinda katika mchezo Wake wa kombe la shirikisho dhidi ya Esparance lakini kiwango chake bado kinaonekana kuyumba hasa katika safu ya ulinzi.

Mwadui ambayo inanolewa na kocha mwenye maneno mengi Jamhuri Kihwelo 'Julio' inawatumia wachezaji wazoefu waliocheza ligi hasa katika klabu za Simba na Yanga kama Jerry Tegete, Athuman Iddi 'Chuji' na Nizar Khalfan ambao ndio silaha kubwa katika kikosi hicho.

Bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha nchi katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika na sio mshindi wa pili wa ligi kama ilivyozoeleka baada ya kuanzishwa tena msimu huu.

Post a Comment

 
Top