BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
Straika wa Big Bullets, Chiukepo Msowoya

NYOTA wa Mabingwa wa Ligi Kuu ya Malawi, Big Bullets na timu ya Taifa ya nchi hiyo, Chiukepo Msowoya na Owen Chaima huenda msimu ujao wakaonekana kukipiga katika klabu ya Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Tayari viongozi wa timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya wameanza kufanya mazungumzo na nyota hao ambapo wamekubaliana kutiliana saini baada ya ligi kumalizika.

Aliyekamilisha dili hilo ni kocha wa timu hiyo Kinnah Phiri ambaye pia ni raia wa Malawi na amewahi kuifundisha timu ya Taifa ya Malawi na amesema kuwa mazungumzo ya awali yamekwenda vizuri na hiyo yote ni kuhakikisha kikosi hicho kinakuwa na upinzani mkubwa msimu ujao.

Kipa wa Bullets, Owen Chaima

"Msowoya ni straika na Chaima ni kipa na wote wanacheza timu moja ya Big Bullets na wapo timu ya Taifa, nawafahamu vizuri na mambo yakienda vizuri basi msimu ujao tutakuwa nao," alisema Phiri.

Ni wazi kwamba, kama dili hilo litakamilika basi Chaima ataziba nafasi ya kipa Juma Kaseja na Msowoya ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa atachukuwa nafasi ya straika Them Felix ambao wote mikataba yao inamalizika msimu huu.

Post a Comment

 
Top