BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu, Mbeya
KOCHA mkuu wa Mbeya City Fc, Kinnah Phiri ametangaza orodha ya nyota 18 watakaokuwa sehemu ya mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara dhidi ya Mtibwa Sugar, uliopangwa  kuchezwa jumamosi hii  Manungu Complex,  Turiani, Morogoro.

Akizungunza na tovuti ya timu hiyo muda mfupi  baada ya kumalizika kwa mazoezi ya asubuhi kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa, Kocha Phiri alisema kuwa hana tatizo na nafasi  ya 10 iliyopo timu yake hivi sasa kwenye msimamo wa ligi kwa sababu anaamini ushindi kwenye michezo miwili ijayo utakifanya kikosi chake kusogea mpaka nafasi ya nane.

“Msimamo wa ligi unaonyesha tuko kwenye nafasi ya 10, hili siyo tatizo sana kwa sababu kushinda mechi mbili zijazo kutatuingiza kwenye timu nane bora, hili ndilo lengo letu, tuna  michezo minne mbele nina uhakika kwamba kila mchezaji anafahamu kuwa tunatakiwa kuongeza pointi zaidi ili tumalize ligi tukiwa sehemu ya timu nane za juu,” alisema Phiri. 

Kocha huyo aliongeza kuwa kwenye mchezo huo wa  Morogoro kikosini atawakosa nyota kama Raphael Daud anayeguza majereha ya mguu, mlinzi Haruna Shamte  aliye kwenye zuio la kucheza kufuatia kadi za njano, huku pia akiwakosa Haruna Moshi 'Boban' na nahodha Temi Felix ambaye  kwa muda mrefu amekuwa nje ya kikosi kutokana na matatizo ya kifamilia.

“Ni wazi hatutakuwa na Boban anayesumbuliwa na malaria, pia Temi alikuwa nje ya timu  akishughulikia masuala ya kifamilia amerudi kambini juzi hivyo kwa vyovyote hawezi kuwa sehemu ya mchezo huo, Raphael ni mgonjwa na Shamte ana  zuio la kadi za njano. Kutokuwepo kwao hakuondoi dhamira yetu ya kushinda mchezo kwa sababu tumekuwa na maandalizi mazuri na muhimu kwa wachezaji wetu wengine ambao sasa wako tayari,” alimaliza Phiri na kutaja baadhi ya nyota wakaosafiri tayari kwa kuivaa Mtibwa Sugar jumamosi hii.

Miongoni mwa nyota  ambao kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Malawi  aliwataja  ni pamoja  na Juma Kaseja, Haningtony Kalyesubhula, John Jerome, John Kabanda, Yusuph Abdalah, Deo Julius, Tumba Lui, Hassan Mwasapili, Kenny  Ally, Hamidu Mohamed na Meshack Samwel  huku akisema  kikosi  chake  kinatarajia kuanza  safari jioni ya leo moja kwa moja  kuelekea  wilayani Turiani.

Post a Comment

 
Top