BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu  Rajabu, Dar 
KOCHA wa Yanga Hans Van Der Pluijm amesema kuwa ushindi wa tabu wa mabao 2-1 walioupata jana dhidi ya Mwadui Fc katika mechi ya kiporo cha ligi kuu ya Vodacom, ulitokana na kujiamini kulikopitiliza kwa wachezaji wake.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa  Taifa jijini Dar es Salaam, Pluijm amesema walipoteza nafasi nyingi sana za kufunga huku wachezaji wake wakionyesha dalili za kujiamini sana na kuidharau Mwadui.

"Nashukuru tumepata ushindi unaotuweka katika mazingira mazuri ya  kutetea ubingwa wetu, ila ni ushindi ambao tumeupata katika mazingira magumu kutoka na wachezaji wangu
 kuwadharau wapinzani wetu, " alisema Pluijm.

Hata hivyo Pluijm ameahidi kuzifanyia kazi kasoro zilizoonekana katika mchezo huo na hivyo kuahidi kikosi kuwa imara pindi watakapocheza na Mtibwa hapo Jumamosi.

Kwa upande wa kocha wa Mwadui Jamhuri Kihwelo "Julio' amemlalamikia mwamuzi kwa kumpa kadi nyekundu mchezaji wake Iddi Mobby hali anayosema ilisababisha kuwatoa wachezaji wake mchezoni .

Julio amesema Yanga haikuwazidi wao kwa ubora isipokuwa walinufaishwa na uchezeshaji mbovu wa mwamuzi Selemani Kinugani wa morogoro na msaidizi namba mbili Haji Mwalukuta wa Tanga ambao amesema walikuwa na maamuzi mabaya dhidi yao .

"Soka la Tanzania lina safari ndefu kutoka na waamuzi kuamini kuwa Yanga,Simba na Azam ndizo pekee zinazostahili hushinda, kama Yanga, mara nyingi inapocheza na timu ndogo lazima mchezaji wa timu pinzani apewe kadi nyekundu au Yanga kupewa penati." alisema Julio.

Post a Comment

 
Top