BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
KOCHA wa makipa wa klabu ya Yanga Juma Pondamali amesema ameleta mapinduzi makubwa katika idara hiyo baada ya kuweka usawa wa kucheza kwa makipa wake.

Pondamali amesema kuwa makipa Ally Mustaph'Barthez'  na Deo Munishi 'Dida' wanapata nafasi sawa za kucheza kitu ambacho hakikuwepo wakati yeye akijiunga na kikosi hicho kama kocha wa makipa 2009.

"Wakati najiunga na Yanga nilimkuta kipa Juma Kaseja akiwa ndiyo chaguo la kwanza lakini nilivyoingia nikabadilisha na kuweka usawa na ndiyo matunda mnayoyaona," alisema Pondamali.

Aidha kocha huyo alikataa kuwalinganisha makipa wake Dida na Barthez na kusema wote ni wazuri na kila mmoja ana nafasi yake ndani ya Yanga.

"Wote ni wazuri na mimi kama kocha  nipo nao muda mwingi na wanajituma sana mazoezini na pia nidhamu zao zinaridhisha," aliongeza.

Pondamali amewahi kuidakia timu ya Yanga miaka ya nyuma na pia alikuwa golikipa wa timu ya taifa iliyoshiriki michuano ya Afrika mwaka 1980.

Post a Comment

 
Top