BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally


MTIBWA Sugar na Prisons zipo kwenye kinyanganyiro cha kushika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kutanguliwa na vigogo Simba, Yanga na Azam lakini leo timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1.

Mtibwa ndiyo walikuwa wenyeji wa Maafande hao katika Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro wamejikuta wakishindwa kuonyeshana umwamba na hivyo kila mmoja kuambilia pointi moja ambayo imeifanya Mtibwa ifikishe pointi 43 na Prisons pointi 41.

Mtibwa Sugar ndiyo ilianza kuona lango la Prisons kupitia kwa mchezaji wao Ramadhan Kichuya wakati bao la kusawazisha la Prisons lilifungwa na Frank William.

Katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mwadui walishindwa kuonyesha ubora wao mbele ya wenyeji Ndanda Fc na kujikuta wakiambulia kichapo cha bao 2-1. Mabao ya Ndanda yalifungwa na Bryason Raphael pamoja na Hamad Msumi huku Mwadui ikifutwa machozi na mchezaji wao Kelvin Sabato.

Kwa matokeo hayo Mwadui wamebaki na pointi zao zile zile 34 wakati Ndanda wenyewe wamefikisha pointi 30 na kujitengenezea mazingira mazuri ya kubaki kwenye ligi msimu ujao.

African Sports pamoja na kuifunga Kagera Sugar bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwaji jijini Tanga lakini bado hali yao ni mbaya katika msimamo wa ligi kwani imebaki nafasi ya 15 ikiwa imefikisha pointi 23. Bao la Sports lilifungwa na 
Hassan Materema, Kagera Sugar wao wanashika nafasi ya 13 wana pointi 25.

Post a Comment

 
Top