BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda


STRAIKA wa KRC Genk na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta leo amefunga bao safi akiisaidia timu yake kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Oostende kwenye dimba la Cristal Arena jijini Genk.

Oostende walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi kali langoni mwa Genk katika dakika ya 11 ambapo shuti kali lililogonga mwamba liligeuka kuwa sumu kwao wenyewe baada ya kunaswa na wachezaji wa Genk waliogongeana kwa kasi na kumkuta Alejandro Pozuelo aliyeiandikia bao la kwanza kwenye dakika ya 12.

Baada ya bao hilo Genk walizidi kuliandama lango la Oostende huku winga mjamaica Leon Bailey akiwa mwiba mkali kwa wageni hao. Hata hivyo Genk walionekana kupoteza mipira mara kwa mara jambo lililowafanya washindwe kukamilisha mipango yao.

Dakika ya 21, Bailey alifanya kazi ya ziada ya kuwakimbiza mabeki wa Oostende na kumpasia nahodha  Thomas Buffel aliyeiandikia Genk bao la pili hivyo kuifanya timu hiyo iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao mawili.

Samatta aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya straika anayeongoza kwa mabao klabuni hapo Nikos Karelis, alifanikiwa kuifungia Genk bao la tatu kwa pasi ya Neeskens Kebano katika dakika ya 76 ya mchezo, huo ukiwa ni mpira wake wa kwanza kugusa tangu aingie dakika ya 75.

Hilo ni bao la tatu kwa Samatta tangu ajiunge na Genk akitokea TP Mazembe ya nchini DR Congo.  Bao la nne la Genk lilifungwa na Kebano katika dakika ya 85.

Ligi kuu ya Ubelgiji imeingia kwenye hatua ya timu sita bora 'Play Off I' ambapo timu sita za juu kwenye msimamo wa ligi iliyomalizika mwezi uliopita ndizo zilizofuzu huku zikiwa zimeingia na nusu ya pointi walizomalizanazo hatua ya awali. Genk inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 27 baada ya kushuka dimbani mara mbili ikipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Anderletch.

Post a Comment

 
Top