BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
STRAIKA aliyeanza kuteka nyoyo za mashabiki wa KRC Genk ya Ubelgiji, mtanzania Mbwana Samatta leo alilazimika kutoka uwanjani katika dakika ya 45 kwenye mchezo wa ligi kuu nchini humo dhidi ya AA Gent baada ya kugongwa na kuumizwa vibaya  puani.

Samatta alikutana na dhoruba hiyo mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili ambapo aligongana na beki wa Gent na kupata maumivu makali yaliyompelekea kushindwa kuendelea na mchezo huku nafasi yake ikichukuliwa na Nikos Karelis.

Taarifa za awali zinasema Samatta amevunjika pua huku mwenyewe akiieleza BOIPLUS kuwa ana maumivu makali sana na leo jumatatu ndipo atapata majibu ya vipimo yatakayoonyesha atalazimika kukaa nje kwa múuda gani.


"Nasikia maumivu makali sana, kwasasa sijajua kama kukaa nje itakuwa ni kwa muda gani, ila kesho (leo) ndio nitajua," alisema Samatta.

Wakati Samatta anatolewa nje, timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1 lakini bao la dakika ya 90 la Renato Neto wa Gent alilopachika wavuni kwa mkwaju wa penati, liliwalaza wenyeji Genk mapema na kupoteza pointi tatu.

Genk inabakia katika nafasi ya nne kwenye ligi hiyo iliyo kwenye hatua ya sita bora (Play Off I) ikiwa imejikusanyia pointi 33 huku vinara Club Brugge wakiwa na pointi 41

Post a Comment

 
Top