BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda

BAADA ya kuifungia bao la tatu KRC Genk, straika Mbwana Samatta amesema kuwa amebakiza mabao matano tu ili atimize lengo alilojiwekea katika msimu wake wa kwanza ndani ya klabu hiyo.

Akizungumza na BOIPLUS kutokea nchini Ubelgiji mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Oostende, Samatta alisema amefurahi kuendelea kuifungia mabao timu hiyo hivyo anaamini malengo yake yatatimia.


"Ni kweli napata dakika chache, lakini hiyo ni mipango ya mwalimu, chamsingi ni kwamba nazitumia vizuri dakika hizo kuipatia mabao timu yangu

" Nilijiwekea malengo ya kufunga mabao manane katika msimu huu ambao nilikuta umeshaanza, kwahiyo hapa nadaiwa matano tu ambayo namuomba Mungu anijalie niweze kufanikisha azma yangu hiyo," alisema Samatta ambaye ni baba wa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Karim.

Samatta ambaye siku zote anaota kuja kuwa mchezaji nyota wa Liverpool ya Uingereza, amefanikiwa kuzoea kwa haraka soka la Ulaya huku akiwateka mashabiki wa Genk kutokana na uhodari wake wa kuziona nyavu.

Post a Comment

 
Top