BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
SIMBA wanafahamu kuwa wana kazi ngumu mbele yao ili watwae ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao wameupotezea kwa zaidi ya miaka mitatu, hivyo ili wawepo kwenye ramani ya kutwaa ubingwa huo ni lazima waifunge Azam wikiendi hii kwani tayari tiketi moja ya kushiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika waliipoteza.

Simba ipo visiwani Zanzibar ambako imepiga kambi sehemu ambayo wanaamini kwamba utulivu wa mazingira utawasaidia kuwaandaa wachezaji wao kuhakikisha wanaifunga Azam ambayo tayari imetinga hatua ya fainali kwenye michuano ya Kombe la FA, mechi ya Simba na Azam itachezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Simba inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kufufua matumaini ya kunyakua ubingwa na kurejesha morali ya wachezaji baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo ya Kombe la FA dhidi ya  Coastal Union na mechi ya ligi dhidi ya Toto African. Simba ilifungwa na Coastal bao 2-1 wakati Toto walishinda pia bao 1-0 katika dimba la Taifa dhidi ya wekundu hao.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jackson Mayanja alisema kuwa hawajakata tamaa ya kutwaa ubingwa na wanayo nafasi ya kufanya hivyo japokuwa kuna ushindani mkubwa toka kwa Yanga na Azam.

Simba imejikusanyia pointi 57 baada ya michezo 25 nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 59 ambao kesho Jumatano watacheza mechi yao ya kiporo dhidi ya Mgambo JKT ambayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa.

Post a Comment

 
Top