BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Dar
KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja amejifariji kwa kutamka kuwa kupoteza mchezo katika soka ni jambo la kawaida huku akisifu kikosi chake kuwa kimecheza vizuri japokuwa wameondolewa kwenye michuano hiyo ya Kombe la FA.

Simba inayoongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 57 imekubali kipigo cha bao 2-1 na vibonde wa ligi hiyo Coastal Union ambao wanashika mkia wakiwa na pointi 19 pekee.

Mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Coastal Union wameungana na Yanga, Azam pamoja na Mwadui FC ya Shinyanga na droo ya nusu fainali itachezeshwa kesho Jumanne saa 4 asubuhi na matokeo yataifanya Simba ibaki na tumaini moja pekee la kupambana kutwaa ubingwa wa ligi.

Mayanja amejitetea kwa kusema kuwa mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo pia alichangia kuwapoteza na kupata matokeo hayo ambayo yamewasikitisha mashabiki wa timu hiyo.

"Mpira ni mchezo wa mkosa, sisi tumeweza kupata nafasi nyingi lakini hatukutumia vizuri, wenzetu wametumia udhaifu huo na kupata matokeo. Pia sikuwatumia baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kwani walichelewa kujiunga na timu akiwemo Hamisi Kiiza," alisema Mayanja.

Kwa upande wa kocha wa Coastal Union, Ally Jangalu alisema: "Tuliweka imani ya kushinda ili kutinga nusu fainali na hilo limewezakana kwa wachezaji wangu kujituma na kupambana katika dakika zote 90,"

Jangalu alisisitiza kuwa hata kwenye ligi wana imani kwamba bado wana nafasi ya kupambana kwani wamebakiza mechi nyingi ambazo wanauwezo wa kushinda na kubaki hivyo mashabiki wa timu hiyo kutokata tamaa. Coastal wamebakiza mechi nne, tatu wanacheza nyumbani na moja ugenini.

Post a Comment

 
Top