BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini(TAKUKURU) imeanza kufuatilia sakata la tuhuma ya rushwa kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza kati ya Polisi Tabora na JKT Oljoro pamoja na Geita Gold Sports dhidi ya JKT Kanembwa ambazo tayari zimeshushwa daraja.

Jana Jumapili, Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ziliishusha Geita, Polisi Tabora na JKT Oljoro kwenye Ligi Daraja la Pili huku JKT Kanembwa ikitupwa ligi ya Mkoa, zote zikituhumiwa kupanga matokeo kwenye mechi zao za mwisho.

Mbali na timu hizo kushushwa madaraja pia, baadhi ya viongozi, wachezaji, waamuzi na makamisaa walifungiwa kujishughulisha na soka katika maisha yao yote huku wengine wakipewa adhabu ya kufungiwa miaka 10 pamoja na kutuzwa faini ya Sh 10 milioni.

Afisa Habari wa Taasisi hiyo, Tunu Mleli amesema kuwa taasisi yao ambayo imepewa dhamana na serikali ya kufuatilia tuhuma za utoaji na upokeaji rushwa vitendo ambavyo vinapigwa vita, imeanza kulifanyia kazi suala hilo.

"Sisi ndiyo wenye dhamana ya kushughulikia wapokeaji na watoaji rushwa, tumesikia juu ya sakata hili na tayari kitengo maalumu kimeanza kufanya kazi yake, hatuwezi kusema tutaanzia wapi ila kazi itafanyika kwa umakini ili kulibaini hili kwani imegundulika rushwa kwenye michezo ni tatizo.

"Katika ufuatiliaji wa sakata la rushwa huwa hatufuatilii kwenye mambo mengine bali ni mambo yote yaliyopo kwenye jamii, hivyo hili ni suala kubwa na hatuwezi kusema litachukuwa muda gani, uchunguzi huwa unafanywa kwa awamu kutokana na ukubwa wa tatizo lenyewe, tukimaliza tutatoa tamko," alisema Tunu.

Post a Comment

 
Top