BOIPLUS SPORTS BLOG

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeishukuru Kampuni ya Bia ya Heineken ambayo pia  ni wadhamini wakuu wa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya (UEFA) kwa kujitolea kufanya ukarabati wa viwanja vitatu vya mpira wa miguu vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Katika barua ya Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Michael Mbugu kwenda kwa wakurugenzi ya Manispaa wilaya za Ilala na kinondoni, nakala yake kutumwa kwa Rais wa TFF, imeeleza kuwa mdhamini ameelekeza nguvu zake kwenye ukarabati wa baadhi ya viwanja nchini ili viwe katika hali nzuri na salama kwa ajili ya kukuza vipaji vya vijana kwenye mchezo wa soka.

Heineken imedhamiria  kushirikiana na jamii kuboresha sehemu mbalimbali kwa kuchangia ukarabati wa viwanja vya TP Manzese kata ya Sinza, Sigara Segerea kata ya Tabata Sigara na uwanja wa Magunia Msasani uliopo kata ya Msasani.

Kufanya ukarabati wa viwanja hivyo kutatoa nafasi kwa vijana wengi toka sehemu mbalimbali hapa jijini kupata nafasi ya kufanya mazoezi kitu kitakachosaidia kuinua vipaji vya soka hasa kutoka mitaani. 

Aidha TFF inazipongeza Halmashauri za Manispaa za Ilala na Kinondoni kwa kupata nafasi ya kufanyiwa ukarabati viwanja vyao na kampuni hiyo na kuziomba mamlaka hizo kuvitunza viwanja hivyo ili viweze kutumiwa na vijana wa kike na kiume katika mchezo wa mpira wa miguu.

Post a Comment

 
Top