BOIPLUS SPORTS BLOG

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezitakia kila la kheri klabu za Azam FC na Yanga ambao ndiyo wawakilishi pekee wa nchi katika michuano ya kimataifa itayochezwa wikiendi hii.

TFF imezitaka klabu hizo kupambana kwa hali na mali katika michezo inayowakabili na kuweza kufanya vizuri kwa kupata ushindi, ili kujitengenezea mazingira mazuri katika michezo ya marudiano itakayochezwa Aprili 19 na 20

Yanga wanacheza hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na  wanashuka dimbani kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam saa 10:00 jioni  kucheza dhidi ya Al Ahly toka Misri katika mchezo namba 89 wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huo utachezeshwa na Dennis Dembele, akisaidiwa na Marius Donatien, Moussa Bayere, mwamuzi wa akiba akiwa Tangba Kambou wote kutoka Ivory Coast, huku kamisaa wa mchezo huo akiwa Celestin Ntangungira kutoka Rwanda.

Katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi keshokutwa Jumapili Azam FC watakuwa wenyeji wa Esperance ya Tunisa katika mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika  hatua ya 16 bora utakaochezwa saa 9 alasiri.

Waamuzi wa mchezo huo namba 75 ni Daniel Frazer Bennet, akisaidiwa na Zakhele Siwela, Thembisile Theophilus na mwamuzi wa akiba akiwa ni  Mbongiseni Fakudze wote kutoka  Afrika Kusini, huku kamisaa wa mchezo akiwa ni Joseph Nkole kutoka  Zambia.

Post a Comment

 
Top