BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar


JANA Jumapili, beki wa Simba, Hassan Kessy alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu straika wa Toto Africans, Edward Christopher na kuisababaisha timu yake kucheza ikiwa pungufu na baada ya mechi hiyo kipa wao Vincent Angban alichukuwa hatua kali ya kumwadhibu kwa kumpiga Kessy kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

Kitendo hicho kiliwakera pia baadhi ya wachezaji wa Simba pamoja na Meneja wa beki huyo, Athuman Tippo ambaye amewataka viongozi wa timu hiyo kuchukuwa hatua za kinidhamu kwa kipa wao vinginevyo wao ndiyo watachukuwa hatua kali juu yake ambapo imeelezwa kwamba wakati yote hayo yakiendelea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, Kessy alikuwa akilia kwa uchungu.

Imeelezwa kwamba Kessy alijikuta akiwaza na kufika mbali kwamba ni vyema akaachana na timu hiyo ili aangalie maisha sehemu nyingine kauli ambayo Meneja wake amemtuliza kwa kutamka kuwa watajadili hilo kwa kina.

Tippo alisema kuwa kitendo cha Angban kumpiga Kessy ni kosa kwani kinamuweka mchezaji mwenzake katika wakati mgumu kwa mashabiki wake na kusisitiza kwamba rafu iliyochezwa ilikuwa ya kimchezo ambapo hata Kessy pia angeweza kuumia endapo angedondoka chini.

"Tunaomba viongozi wa Simba wachukue hatua kwa Angban, wasipochukuwa hatua yoyote sisi tutachukuwa hatua kwani alichokifanya Angban ni kosa, Kessy kafanya makosa ya kimpira ambayo hata yeye anayafanya kwani mara kadhaa amekuwa akifungwa magoli ya kizembe ila hakuna mchezaji anayempiga.

"Ni kweli Kessy anamaliza mkataba wake ila tutakaa naye chini ili amalizane nao vizuri, kitendo hiki kimemuumiza ndio maana amekata tamaa ya kuendelea kuwepo, lakini tutazungumza nae ili aachane nao kwa kufuata taratibu zinazotakiwa," alisema Tippo.


Kessy ameonekana kuumizwa na kitendo hicho ambapo yeye ametamka kwamba kila kitu amemwachia Mwenyezi Mungu kwani ndiye mwenye kupanga.

Jana Edo aliiambia BOIPLUS: "Katika mpira kuna vitu kama hivyo huwa vinatokea, mara nyingi inakuwa ni ubabe tu wa uwanjani ili kila mmoja amshinde mpinzani wake ndivyo ilivyotokea kwa Kessy na siwezi kusema kama amefanya makusudi naamini ni bahati mbaya tu.

''Nilijikuta tu nipo chini, sikupoteza fahamu bali kifua ndo kilikuwa kimebana sana na kusikia maumivu makali, kama alifanya makusudi nimemsamehe kwani yule ni mdogo wangu.

"Niliingia kucheza ila baadaye nilishindwa kutokana na maumivu makali niliyokuwa naendelea kuyasikia ndiyo maana niliomba kutoka nje. Ila mashabiki watambue kwamba Kessy ni rafiki yangu na wala siwezi kumchukia kwa hili," alisema Edo.

Post a Comment

 
Top