BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Simba 'Wekundu wa Msimbazi' wamepata pigo katika harakati za kuutafuta ubingwa wa ligi kuu ya Bodacom baada ya kukubali kichapo cha goli 1-0 toka kwa Toto African ya Mwanza kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam .

Simba waliianza mechi hiyo kwa kasi ambapo dakika ya pili ya mchezo mshambuliaji Danny Lyanga alipiga shuti kali lililotoka nje kidogo ya lango la Toto.

Simba waliendelea kuliandama lango la Toto na dakika ya 10 shuti hafifu ambalo lilionekana halina madhara lililopigwa na Lyanga tena liligonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani ambapo ingeweza kuwapa wekundu hao goli la uongozi.

Toto ambao walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza na kutumia mipira mirefu walifanikiwa kupata goli la kuongoza dakika ya 21 kupitia kwa Waziri Junior aliyepiga shuti kali lililomshinda golikipa Vicent Agban na kutinga wavuni. Waziri aliutumia vema mpira mrefu uliogongwa kichwa na Edward Christopher na kumkuta yeye akiwa kwenye nafasi nzuri.

Dakika ya 30 Kocha wa Simba Jackson Mayanja alitolewa nje na mwamuzi Ahmed Simba toka Kagera baada ya kutoa lugha isiyofaa kutokana na mchezaji wake kufanyiwa madhambi na mchezaji wa Toto.

Mpaka timu hizo zinaenda mapumziko Toto walikuwa mbele kwa goli moja

Dakika moja baada ya kuanza kipindi cha pili beki Hassani Kessy alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Edward Christopher.

Baada ya kadi hiyo Simba walifanya mabadiliko ya kumtoa Musa Mgosi na kumuingiza Emery Nimuboma ili kuongeza kasi upande wa kulia.

Dakika ya 55 Toto walifanya mabadiliko ya kumtoa Juma Saidi nafasi yake ikichukuliwa na Salmin Hozza na dakika moja baadae Simba walifanya mabadiliko ya kumtoa Peter Mwalyanzi na kumuingiza Ibrahim Ajib ambaye aliongeza kasi kwa upande wa Simba.

Licha ya kuwa pungufu Simba waliendelea kulisakama lango la Toto mara kadhaa lakini mlinda mlango Musa Kirugi alikuwa kikwazo.

Dakika ya 70 Toto walifanya mabadiliko ya kumtoa Edward Christopher na Japhar Mohammed na kuwaingiza Japhet Vedastus na William Kimanzi.

Mpaka dakika tisini za mchezo zinakamilika Toto African 'wana kishamapanda' wameondoka na ushindi wa goli 1-0

Simba wamebakia na pointi zao 57 na kuendelea kushika nafasi ya pili baada ya kushindwa kuwashusha Yanga kileleni wakiwa na alama 59.

Post a Comment

 
Top