BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
MASTRAIKA wawili wa TP Mazembe ya DR Congo, Thomas Ulimwengu na Christian Luyindama leo wametokea benchi na kuiwezesha timu yao kupata ushindi wa mabao 2-0 kwenye mechi ya ligi kuu nchini humo dhidi ya Shark XI Fc iliyopigwa kwenye dimba la Stade Des Martyrs, Kinshasa.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana licha ya kosakosa kadhaa.

Kipindi cha pili Ulimwengu na Luyindama waliingia kuchukua nafasi za Roger Assale na Given Singuluma katika dakika za 57 na 59. Mabadiliko hayo ndiyo yaliyoiwezesha Mazembe kuibuka na pointi tatu katika mechi ya ligi hiyo iliyo kwenye hatua ya nane bora (Play Offs).

Dakika ya 65, Luyindama aliitumia vema pasi ya Bolingi kuiandikia Mazembe bao la kwanza ambapo dakika tatu baadae Ulimwengu alipachika bao la pili baada ya kazi nzuri ya Rainford Kalaba.

Kwa matokeo hayo Mazembe wamefika nafasi ya nne baada ya kujikusanyia pointi 9 kwa michezo yao mitatu waliyocheza. Vinara wa ligi hiyo Sanga Balende wana pointi  12 huku akiwa ameshashuka dimbani mara tano.

Mazembe watarejea jijini Lubumbashi kesho ili kujiandaa nachezo wa marudiano wa ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Athletic Club  ambapo katika mchezo wa awali uliochezwa nchini Morocco Mazembe walilala kwa mabao 2-0

Kikosi cha Mazembe kilikuwa hivi;
 Gbohouo, Frimpong, Kimwaki (C), Bope, Kasusula, Sinkala, Adjei (Kouame dak 77), Singuluma (Luyindama dak 59), Assale (Ulimwemgu dak 57), Bolingi, Kalaba.

Post a Comment

 
Top