BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar
SAFARI ya kiungo wa Azam, Himid Mao kwenda Ulaya ilikwama baada ya kushindwa kupata Visa yake kwa wakati kufuatia hati yake ya kusafiria kuchelewa kwenye Ubalozi wa Tunisia ambako ilipelekwa kwa ajili ya safari ya timu yake ilipokuwa inaelekea kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Esperance.

Mao alitakiwa kwenda nchini Denmark April 22 kwa ajili ya majaribio wakati mwenzake Farid Musa tayari alikwenda Hispania atakakofanya majaribio ya mwezi mzima katika timu mbili za Atletic Bilbao na Las Palmas.

Akizungungumza na BOIPLUS, Himid alisema baada ya kushindwa kuondoka analazimika kusubiri apangiwe tarehe nyingine ili aende kujaribu bahati yake.


"Mambo yaligongana, wakati tunajiandaa kwenda Tunisia ndicho kipindi nilipaswa kupeleka 'Paspoti' yangu ubalozi wa Denmark kwa ajili ya kugonga VISA, ndio sababu ilishindikana. Nasubiri wanipangie tarehe nyingine tu," alisema Himid ambaye aligoma kuweka wazi timu anayokwenda kufanya majaribio hayo.

Mao alifafanua juu ya hatima yake kwenda Denmark kwamba: "Hiyo timu iliyoniita inapambana kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Europa, hivyo kwasasa ratiba yao imebana sana, nadhani watasubiri hadi wamalizie mechi chache zilizobaki ndipo niende."

Endapo Farid na Himid watafanikiwa kusajiliwa baada ya majaribio yao huku mipango ya Thomas Ulimwengu kutimkia Ulaya ikifanikiwa basi Tanzania itajivunia kuwa na wachezaji wanne wanaocheza soka la kulipwa kwenye bara hilo linaloongoza kwa soka duniani akiwemo Mbwana Samatta ambaye ametangulia.

Post a Comment

 
Top