BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
BAADHI ya wanachana wa matawi ya Simba wamelaani vikali vitendo vya mashabiki wa timu hiyo kumfanyia fujo Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe pamoja na kipa Vincent Angban kumpiga Hassan Kessy kwamba ni kinyume na sheria.

Mwenyekiti wa tawi maarufu na lenye nguvu la timu ya Simba 'Muchacho Group Kidedea', Kibaja Omari Kibaja amesema kukosekana mshikamano ndani ya klabu hiyo ndio chanzo cha kufanya vibaya kwa timu hiyo.

Kibaja alisema kumekuwa na upinzani ndani ya klabu na wanachama mpaka inafikia hatua timu yao inashindwa kushiriki michuano ya kimataifa kwa miaka minne mfululizo.

"Sikufurahishwa na kitendo cha Hans Poppe kufanyiwa fujo na pia kipa kumpiga mchezaji mwenzake ni kitu ambacho kinaongeza ufa ndani ya timu na kipindi hiki ambacho tunahitaji ubingwa tunatakiwa tushikamane," alisema Kibaja.
Mwandishi wa Boiplus akizungumza na mwenyekiti wa Muchacho, Kibaja Kibaja (kulia)

Kwa upande wa mjumbe wa tawi la Simba Manzese Agentina  Feisal Jabir alisema uongozi uliopo madarakani ndiyo chanzo kikubwa kwa timu hiyo kufanya vibaya kutokana na kutofanyia kazi maoni wanayopewa na viongozi wa matawi.

Feisal alisema viongozi wanaendesha timu kwa ubabe na hawashauriki kikubwa ni kuifanya klabu kuwa ni kitega uchumi chao na kufanya mambo yao binafsi.

"Ukiangalia katika wilaya ya Kinondoni kuna matawi 31 lakini kati yao matawi 15 hayakubaliani na uongozi uliopo madarakani na uongozi haujafanya jitihada zozote kuyarudisha kundini matawi hayo kitu ambacho kinaongeza mpasuko ndani ya klabu," alisema Feisal.

Akizungumzia kuhusu fedha za mauzo ya wachezaji Emmanuel Okwi na Mbwana Samatta mjumbe huyo alisema wanachama wanapigwa kiini macho kwa kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa timu hiyo uliopo Bunju mwisho wa siku hakuna kitachofanyika.

" Hakuna kitachofanyika na mabilioni hayo yataliwa na wachache juu kwa juu na suala la uwanja litapigwa danadana," alisema Feisal.

Post a Comment

 
Top