BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
MBEYA City ipo jijini Tanga ikikabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Mgambo JKT lakini kocha wa timu hiyo, Kinnah Phiri ameendelea kusisitiza kuwa ni mechi ya kupata pointi kwake ili mazingira yao ya kubaki Ligi Kuu Bara yawe mazuri.

Mbeya City wana pointi 27, kimahesabu ikishinda mechi hiyo angalau itakuwa imejinasua kwenye hatari ya kushuka daraja wakati Mgambo wao hata wakishinda watafikisha pointi 26 kwani hadi sasa wana pointi 23 hivyo bado watakuwa na kibarua kigumu cha kupigania kutoshuka daraja.

City yenye maskani yake jijini Mbeya imesafiri kilomita 900 kufika Tanga wakiwa na tumaini moja tu la kupata ushindi lakini Phiri ameitazama kwa jicho la nyongeza mechi hiyo na kutamka kuwa mchezo kwao ni mgumu hasa baada ya wapinzani wao kupoteza mechi iliyopita.

"Mji huu una joto sana hata mechi iliyopita tuliyocheza hapa na African Sports tulikumbana na hali ngumu ya joto kwani tulichelewa kufika tofauti na sasa angalau tutaweza kuzoea mazingira. Hii mechi ni ngumu ila tunahitaji kujitoa sana ili tupate ushindi mkubwa ama kutoka sare ila tusipoteza kabisa," alisema Phiri.

Kwa upande wa daktari wa timu hiyo, Joshua Kaseko, alisema "Wachezaji wote tuliosafiri nao wapo vizuri kiafya na mazoezi watakayofanya yatarejesha zaidi uimara wa misuli kwa baadhi ya wachezaji ambao miili yao itakuwa imepatwa na uchovu mkubwa, kuwasili mapema kumetusaidia kwa sababu katika hali ya kawaida mchezaji anapasa apate japo saa 24 za  kupumzika kabla ya kuingia kwenye mchezo."

Post a Comment

 
Top