BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu
KWA kawaida nchi za kiarabu zinasifika kwa kufanya fitina za kuwavuruga wapinzani wao kwenye soka ili wapate ushindi kiurahisi na wengi walitarajia kwamba Yanga wangekutana na fitina hizo lakini hali imekuwa shwari katika jiji la Alexandria, jijini Misri.


Yanga ipo jijini humo kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya michuano ya kimataifa ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Al Ahly itakayochezwa kesho Jumatano ambapo mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Akizungumza na BOIPLUS, Meneja wa timu ya Yanga, Hafidh Saleh alisema kuwa hawajakutana na fitina yoyote ya nje ya uwanja tangu wafike jijini humo hali ambayo inaonyesha kwamba kuna mabadiliko makubwa katika soka barani Afrika kwani awali timu zinazotoka nje ya nchi hizo zilikuwa zikifanyiwa vurugu kuanzia uwanja wa Ndege.

"Wachezaji wote wako vizuri na morali ipo juu wanafanya mazoezi tayari kujiwinda na mchezo wetu wa kesho, hali ya hewa ni ya baridi kiasi na hakuna fitina zozote tulizokutana nazo,'' alisema Hafidh.

Meneja huyo alisema wamepata sapoti kubwa toka ubalozi wa Tanzania nchini Misri pamoja na watanzania wanaoshi huko ambao huwatembelea hotelini na wanapofanya mazoezi.

Post a Comment

 
Top