BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Dar
KIVUMBI cha Ligi Kuu ya Vodacom kinaendelea kutimua vumbi wikiendi hii ambapo kutakuwa na mechi tatu zitakazochezwa kwenye viwanja vitatu tofauti.

Mechi ambayo inatazamiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi ni ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Yanga inaikaribisha Mtibwa Sugar ikiwa ni mechi yao ya kiporo.


Mechi hiyo ni ngumu kwa Yanga ambayo inaondoka kesho kuelekea Misri kwa ajili ya mechi yao ya kimataifa ya marudiano dhidi ya Al Ahly ambapo Yanga inapigania ushindi ili iweze kuishusha Simba kileleni. 


Simba ambao kesho Jumapili wana kibarua cha kuifunga Toto Africans kwenye Uwanja huo wa Taifa ndiyo wanaoongoza ligi wakiwa na pointi 57 wakati Yanga wana pointi 56 huku Azam wenyewe wakikusanya pointi 55.Yanga haijapoteza mchezo wowote katika uwanja huo msimu huu huku takwimu zikionesha katika michezo yao mitano ya mwisho imeshinda michezo mitatu na kutoka sare miwili mmoja wao ukiwa ni ule wa Azam ambapo uliisha kwa sare ya mabao 2-2.


Katika mchezo dhidi ya Mwadui, Yanga ilikosa umakini katika idara ya ulinzi kutokana na kutokuelewana vizuri kwa mabeki wa kati ambapo nahodha Nadir Haroub 'Canavaro' alicheza na Pato Ngonyani na kufanya makosa mengi kabla ya kocha Hans van der Pluijm kufanya mabadiliko ya kumtoa Ngonyani na kumuingiza Vincent Bossou.


Safu ya ushambuliaji pia imeonekana kutofanya vizuri sana siku za hivi karibuni baada ya kuwa wanapoteza nafasi nyingi za kufunga kitu ambacho kinaweza kuwagharimu kwenye mechi hiyo.


Nguvu kubwa ya Mtibwa Sugar inayonolewa na Mecky Maxime ni katika safu ya kiungo ambayo ipo chini ya mkongwe Shabani Nditi, Mohamed Ibrahim na Mohamed Rajabu 'Jeba' ambao wanacheza kwa uelewano mkubwa kitu ambacho kinaweza kuwa kikwazo kwa wachezaji wa Yanga.Upande wa kulia ambapo anacheza Shiza Kichuya nako kutakuwa na kazi kubwa kwakuwa atakutana na beki Mwinyi Haji au Oscar Joshua ambao wote viwango vyao haviko sawa sawa baada ya kutoka kwenye majeruhi.


Mtibwa imeshuka dimbani mara 25 na imefanikiwa kukusanya pointi 43 ambazo zimewaweka kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo.


Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema "Tunauchukulia kwa uzito wake mchezo huo kwani utatoa ramani ya ubingwa, Mtibwa ni timu ngumu na wanacheza kitimu kitu ambacho ni faida kwao."


Kwa upande wa Maxime alisema kuwa  wamekuja Dar es Salaam kusaka alama tatu japokuwa haitakuwa rahisi kutokana na wapinzani wao kuwa katika mbio za ubingwa lakini wao hawatakubali kufanywa daraja na Yanga.


Mechi nyingine itachezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ambapo vibonde Coastal Union watawakaribisha JKT Ruvu.

Post a Comment

 
Top