BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu
YANGA wameondolewa kwenye michuano ya Mabingwa Afrika na sasa watakutana na Grupo Desportivo Sagrada Esperance ya Angola katika hatua ya makundi  ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

Yanga wametolea na Al Ahly ya Misri kwa kukubali kichapo cha mabao 2-1 hivyo wataanzia mechi yao nyumbani ambapo mechi hiyo itachezwa Mei 8 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Mwalimu J. K. Nyerere na Ndege ya Shirika la Ethiopia, wametamba kumaliza ubishi kwa Waangola huku wakionyesha kuwa na hamu kubwa ya kupambana na Waarabu ambao hawajapangwa nao kwenye michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema ''Tunatamani kucheza na Waarabu ili tuweke heshima tungekutana nao tena kwenye michuano ya Shirikisho. Al Ahly walitufunga kwa kutumia mbinu nyingi nje ya uwanja na si kisoka. Tuna morali kubwa ya kupambana naamini hata hao Waangola tutawafunga na kusonga mbele, tulijitahidi kupambana ila bahati haikuwa yetu,''

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema: "Kwa sasa tunaelekeza akili zetu kwenye mechi ya FA dhidi ya Coastal Union, hatuna shaka na mchezo wa kimataifa na Waangola pia tutafanya vizuri.''

Yanga imekwenda kambini moja kwa moja kujiandaa na mechi hiyo itakayochezwa keshokutwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Post a Comment

 
Top