BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma
YANGA imedhihirisha kuwa wanaweza. Wameifunga Kagera Sugar bao 3-1 katika mechi zao za viporo za Ligi Kuu Bara huku Azam wao wakibanwa mbavu na Toto Africans ya jijini Mwanza kwa kutoka sare ya bao 1-1.

Yanga iliikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na hivyo kufikisha pointi 53 wakati Azam yenyewe ilikuwa ugenini hivyo imefikisha pointi 51. Yanga na Azam wamebakiza mechi mbili za viporo ili kufikisha mechi 24 ambao tayari Simba wanaongoza kwa pointi 57 wamecheza.

Kagera Sugar ndiyo ilikuwa ya kwanza kutikisa nyavu za Yanga kupitia kwa Mbaraka Yusuph dakika ya tisa tangu kuanza kwa mchezo huo ambapo Donald Ngoma aliisawazishia timu yake dakika ya 25.

Yusuph alifunga bao hilo akitopokea krosi safi ya Babu Ally wakati Ngoma yeye alifunga bao hilo kwa kichwa akipokea krosi ya Juma Abdul na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha kwanza Yanga walipata kona tatu ambazo zote walishindwa kuzitumia huku Mwamuzi wa mechi hiyo Erick Unoka wa Arusha akitoa kadi ya njano kwa Babu Ally baada ya kumchezea rafu Amissi Tambwe, Kevin Yondani naye alizawadi kadi hiyo kwa kumfanyia mchezo mchafu Daud Jumanne huku kadi nyekundu ikienda  kwa Shaban Ibrahim.

Yanga ilipata penalti dakika ya 34 baada ya Ngoma kuangushwa eneo la hatari na Ibrahim, penalti hiyo na Yondani lakini shuti lake halikuzaa matunda kwa Yanga. Shuti la Tambwe lililopigwa dakika ya 37 lilitoka nje huku Salum Telela naye akipiga shuti dakika ya 40 na kugonga mwamba.

Hiyo ilikuwa ni kadi ya pili ya njano baada ya kumsukuma kwa makusudi Haji Mwinyi na hivyo kulazimika kupewa kadi nyekundu na timu yake kucheza ikiwa pungufu kuanzia dakika ya 47 huku Mwinyi naye akipewa kadi ya njano.

Kocha wa Kagera Sugar, Adolf Rishard aliamua kufanya mabadiliko baada ya mchezaji wake kupewa kadi ya njano ambapo aliwatoa Martin Lupart na Paul Ngayoma pamoja na Yusuph nafasi zao zilichukuliwa na Ibrahim Job, Idd Kurachi na Ramadhan Kiparamoto.

Naye kocha wa Yanga, Hans Pluijm alifanya mabadiliko ambapo aliwatoa Deus Kaseke, Tambwe na Telela nafasi zao zilichukuliwa na Geofrey Mwashiuya ikiwa ni dakika ya 60 pamoja na Paul Nonga dakika ya 78 pamoja na Pato Ngonyani.

Dakika ya 61, Tambwe aliipatia Yanga bao la pili baada ya kupokea pasi safi ya Simon Msuva wakati shuti la Abdul lililopigwa dakika ya 65 likigonga mwamba na kurudi uwanjani huku mwamuzi akiendelea kugawa kadi za njano ambapo Mwashiuya alipata kadi hiyo kwa kujiangusha eneo la hatari.

Kwa bao hilo Tambwe amefikisha mabao 18 ikiwa ni nyuma ya bao moja ya kinara wa mabao Mganda, Hamisi Kiiza wa Simba mwenye mabao 19 huku Mwinyi akiongeza bao la tatu ikiwa ni dakika ya 87 akifungwa kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Msuva

Matokeo ya mechi nyingine, Stand imeifunga Mgambo JKT bao 2-0, bao la Stand limefungwa na Elius Maguli na hivyo kufikisha mabao 11 sawa na Jeremia Juma wa Prisons bao la pili lilifungwa na Vitaris Mayanga akipokea krosi ya Maguli.

Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, JKT Ruvu wao wamempiga African Sports ya jijini Tanga bao 1-0, bao hilo lilifungwa na Musa Kiumbu ambaye baadaye alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mchezaji wa Sports.

Katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, wenyeji Ndanda FC waligawana pointi na Prisons ya jijini Mbeya baada ya kutoka suluhu.

Post a Comment

 
Top