BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
MABINGWA watetezi wa Ligi Bara, Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui FC na kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea taji hilo baada ya kuzidiwa alama moja na vinara Simba. Mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ambayo ilianza kwa kasi ambapo dakika ya kwanza Amissi Tambwe alipiga kichwa mpira wa krosi ya Simon Msuva lakini golikipa Shabani Kado alikuwa makini langoni na dakika mbili baadaye Simon Msuva aliiandikia Yanga bao la kwanza baada ya kumalizia kwa kichwa krosi ya Oscar Joshua upande wa kushoto kutokana na uzembe wa mabeki wa Mwadui.

Dakika ya 13 mshambuliaji Kelvin Sabati aliisawazishia Mwadui kutokana na kutokuelewana kwa mabeki wa kati wa Yanga Nadir Haroub 'Canavaro' na Pato Ngonyani na kubaki na mlinda mlango Deo Munishi na kufunga goli jepesi.

Yanga waliendeleza kasi na dakika ya 26 Donald Ngoma alifanya kazi ya ziada kuwahadaa mabeki wa Mwadui na kupiga krosi ambapo Tambwe alipiga shuti ambapo lilipaa juu ya lango.

Mwadui nao walifanya shambulio la hatari langoni mwa Yanga dakika ya 28 na kama sio jitihada binafsi za Dida ambapo Sabati angewapitia goli la kuongoza.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko ya kumuingiza Vincent Bosou kuchukua nafasi ya Pato Ngonyani ambaye hakuwa katika ubora na Gofrey Mwashiuya kuchukua nafasi ya Issoufou Boubacar na kuwafanya mabingwa hao kucheza vizuri hasa katika idara ya ulinzi.

Mwadui walimuingiza Nizar Khalfani dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Hassani Kabunda ambaye alicheza vizuri upande wa kushoto na dakika ya 69 beki Iddy Mobby alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Ngoma.

Dakika ya 86 Haruna Niyonzima aliipatia Yanga goli la ushindi baada ya kupiga shuti kali ndani ya eneo la hatari ambalo lilimshinda Kado.

Yanga sasa wamefikisha pointi 56 wakati Simba wana pointi 57. Yanga wana mechi moja ya kiporo mkononi. Azam wao wamejikusanyia pointi 55 baada ya kuitandika Mtibwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Manungu. Bao la Azam lilifungwa na John Bocco katika dakika 62 kwa mkwaju wa penati.


Post a Comment

 
Top