BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
MABINGWA wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Yanga imerejea kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuwafunga wakata miwa wa Mtibwa Sugar kwa goli 1-0 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Mechi hiyo ya kiporo ilipoteza ladha kutokana na uwanja kujaa maji baada ya mvua kubwa kunyesha siku ya leo huku wachezaji wa timu zote wakianguka mara kwa mara na mipango ya timu zote ikishindwa kukamilika.


Hata hivyo Yanga ndiyo walifanya mashambulizi ya mapema ambapo dakika ya saba Haruna Niyonzima aliwapiga chenga mabeki wa Mtibwa na kupiga krosi iliyomkuta Juma Abdul na kupiga shuti ambalo lilipaa juu ya lango.


Dakika ya 25 Simon Msuva alifanya kazi ya ziada kwa kuwahadaa mabeki wa Mtibwa na krosi yake ilimzidi kasi Donald Ngoma akashindwa kuiandikia Yanga goli la kuongoza.


Hadi timu hizo ninaenda mapumziko zilikuwa hazijafungana.Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko ya kumtoa Kelvin Yondani na kumuingiza Malimi Busungu na dakika moja baadae Simon Msuva aliipatia Yanga goli la kwanza kwa shuti kali lililomshinda kipa Said Mohamed. Mpira huo ulitokana na adhabu ndogo  iliyopigwa na Haruna Niyonzima.


Baada ya goli hilo Yanga waliendelea kulisakama lango la Mtibwa lakini mabeki wake wakiongozwa na Andrew Vincent na Salum Mbonde waliweza kuwadhibiti huku golikipa Mohamedi akiwa makini sana langoni.


Kwa ushindi huo Yanga wamefikisha alama 59 ikiwa ndio vinara wa ligi hiyo ikiwashusha Simba hadi nafasi ya pili kwa pointi zao 57.

Post a Comment

 
Top