BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma
WAWAKILISHI wengine wa Tanzania katika michuano ya kimataifa timu ya Yanga wameshindwa kusonga mbele baada ya kukubali kichapo cha magoli 2-1 toka kwa Al-Ahly ya Misri katika mechi ya marudiano ya klabu bingwa barani Afrika.

Katika mchezo huo uliokuwa wa kasi, timu zote zilijitahidi kushambulia na kukaba kwa pamoja ili kuzuia nyavu zao zisiweze kutikiswa katika dakika za awali ili wasitoke mchezoni huku zikicheza kwa tahadhari kubwa na umakini wa hali ya juu.

Dakika ya nne winga Simon Msuva aliambaa na mpira upande wa kushoto na pasi yake ya mwisho kwenda kwa Donald Ngoma ilizuiwa na beki wa Al-Ahly na kupeleka mashambulizi langoni kwa Yanga kabla golikipa Deogratius Munishi 'Dida' hajadaka shuti kali la mshambuliaji Amri Gamal.

Viungo wa Yanga Haruna Niyonzima na Thabani Kamusoko walicheza vizuri eneo la katikati ya uwanja kwa kukaba na kupandisha timu mbele na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwanyima viungo wa Al-Ahly
 nafasi ya kumiliki mpira.

Pamoja na mashambulizi na kosa kosa za hapa na pale timu hizo zilienda mapumziko zikiwa hazijafungana.

Kipindi cha pili dakika ya 51 Al-Ahly walipata goli baada ya mpira wa kona uliopigwa na Moem Zakaria kufungwa na Hosam Ghaly kwa kichwa baada ya kuwazidi ujanja wachezaji wa Yanga na kuruka akiwa peke yake .

Baada ya goli hilo Yanga walirudi mchezoni na kuendelea kulisakama lango la wenyeji wao ambapo dakika ya 66 Donald Ngoma aliisawazishia Yanga kwa goli safi la kichwa baada ya kupokea krosi ya Juma Abdul upande wa kulia .

Ikiwa imebaki dakika moja katika muda wa nyongeza huku watu wakiamini mechi itamalizika kwa sare ya goli 1-1, Al-Ahly walifanya shambulizi langoni kwa Yanga na Abdallah Said aliipatia timu yake goli la ushindi baada ya kupokea krosi safi toka kwa Walid Souliman ambaye aliingia toka benchi na kuwasaidia wenyeji kusonga mbele katika hatua inayofuata.

Licha ya kutolewa Yanga walicheza vizuri kwa muda wote wa mchezo na kutoa upinzani wa kweli kwa wabingwa hao wa kihistoria wa kombe hilo.

Hata hivyo, licha ya kutolewa Yanga itajumuishwa katika timu zitakazohusishwa kwenye droo ya 16 bora ya kombe la shirikisho (CCC) hapo kesho.

Post a Comment

 
Top