BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu
KIKOSI cha Yanga ya jijini Dar es Salaam leo kimejikusanyia alama tatu muhimu baada ya kuifunga Toto Africans mabao 2-1 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza.

Toto ndio walikuwa wa kwanza kufanya sherehe baada ya William Kimanzi kuipatia timu hiyo bao katika dakika ya 39 akimalizia kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na kiungo Abdallah Seseme. 

Bao la Toto lilidumu hadi mapumziko lakini kipindi cha pili Yanga walikuja wakionekana dhahiri kuwa wamepania kusawazisha baada ya kuanza kucheza mpira kasi na kulishambulia lango la Toto mara kwa mara.

Dakika ya 50, Amissi Tambwe aliisawazishia Yanga huku akifikisha mabao 19 sawa na Hamis Kiiza wa Simba. Juma Abdul akaihakikishia ushindi Yanga kwa bao safi katika dakika ya 77 akimalizia kwa shuti kali mpira uliookolewa na mabeki baada ya kipa wa  Toto kuutema.

Kwa ushindi huo Yanga imefikisha alama 75 hivyo kuendelea kuzitimulia vumbi Azam na Simba zitakazopambana kesho katika uwanja wa Taifa.

Matokeo ya michezo mingine ya ligi kuu iliyochezwa leo ni kama ifuatavyo:
African Sports 1-0 Coastal Union
Mwadui Fc 2-1 Stand United
Prisons 1-1 JKT Ruvu
Mtibwa Sugar 1-0 Mbeya City 

Post a Comment

 
Top