BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
YANGA imeendelea kujikita kileleni mwa Ligi Kuu Bara baada ya kuilaza Mgambo JKT bao 2-1 katika mechi ya kiporo iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hivyo kufikisha pointi 62 na kuiacha Simba ikiwa na pointi 57, zote zimebakiza mechi tano kila moja.

Mgambo ndio walikuwa wa kwanza kuliona lango la Yanga dakika ya tatu tangu kuanza kwa mchezo huo bao lililofungwa na Bolly Ajaly wakati Yanga ilisawazisha dakika ya 43 kupitia kwa Deus Kaseke akimalizia krosi ya Simon Msuva.

Kaseke aliongeza bao la pili dakika ya 72 ikiwa ni piga nikupiga langoni mwa Mgambo JKT. Matokeo hayo yanaifanya Mgambo iendelee kuwa katika hali ngumu ya kushuka daraja kwani wamecheza mechi 27 na kukusanya pointi 23 huku ikishika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi.

Straika wa Yanga, Paul Nonga na Amissi Tambwe walionekana kutokuwa na bahati ya kutikisa nyavu kipindi cha kwanza kwani walikosa mabao mengi ya wazi, Nonga alikosa zaidi ya mabao mawili moja likigonga mwamba wakati Tambwe pia akikosa mabao mawili.

Dakika ya 20, kocha wa Yanga aliamua kufanya mabadiliko baada ya kiungo wake Salum Telela kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ilichukuliwa na Mbuyu Twite. Pluijm aliwatoa pia Haruna Niyonzima na Nonga na kuwaingiza Donald Ngoma pamoja na Thaban Kamusoko.

Kocha wa Mgambo, Joseph Lazaro naye alifanya mabadiliko kwa kumtoa Nassoro Gumbo nafasi yake ilichukuliwa na Ally Nassoro.

Mwamuzi wa mchezo huo Alex Mahagi alitoa kadi za njano kwa Telela na Nadir Haroub 'Canavaro' (Yanga) kwa kuwachezea rafu wachezaji wa Mgambo, Said Hamis (kipa wa Mgombo) kwa kupoteza muda, Salum Kipaga

Baada ya mechi hiyo kesho Yanga wanatarajia kuondoka na Fastjet kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi yao na Toto itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo.

Post a Comment

 
Top