BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitangaza timu ya Mbao FC ya jijini Mwanza kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao kutoka katika kundi C la Ligi Daraja la Kwanza nchini (StarTimes League).

TFF imeitangaza Mbao kufuatia maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF yaliyotolewa mapema mwezi huu ya kuzishusha daraja timu nne kutoka kundi C baada ya kukutwa na hatia ya upangaji matokeo.

Mbao imeshika nafasi ya kwanza kundi C kwa kuwa na pointi 12 baada ya kufutwa kwa matokeo ya timu za Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Oljoro na JKT Kanembwa zilizokumbwa na mkasa huo wa upangaji matokeo.

Timu hiyo inapanda ligi kuu msimu ujao sambamba na timu za African Lyon ya jijini Dar es salaam pamoja na Ruvu Shooting ya mkoani Pwani.

Wakati huo huo kikao cha Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya TFF kinatarajiwa kukaa Jumamosi ijayo April, 30 jijini Dar es salaam kujadili rufaa mbalimbali ambazo zimekatwa kutokana na maamuzi ya kamati ya Nidhamu ya TFF.

Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya TFF itasikiliza rufaa za wafuatao;

(i) Saleh Mang’ola,

(ii) Yusuph Kitumbo,

(iii) Amos Mwita,

(iv) Fateh Remtullah,

(v) Timu ya JKT Oljoro,

(vi) Timu ya Polisi Tabora.

Aidha Kamati ya Nidhamu ya TFF itakutana Jumapili Mei Mosi kupitia taarifa mbalimbali zilizowasilishwa katika kamati hiyo.

Post a Comment

 
Top