BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
RAIS wa klabu ya Simba Evans Aveva ametaja mambo manne yaliyoiangusha timu yake mpaka ikashindwa kunyakua ubingwa msimu huu.

Aveva alisema shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF limechangia kutokana na upangaji mbovu wa ratiba ambao umekuwa ukifanya baadhi ya timu kuwa nyuma kwa michezo minne kitu kinachorahisisha upangaji wa matokeo.

Rais huyo pia aliwataja waamuzi kuwa sababu ya Wekundu hao kukosa ubingwa msimu huu kwakua walionekana kuingia uwanjani wakiwa na matokeo mfukoni na ameishauri TFF katika mechi za watani wa jadi marefa watoke nje ya nchi ili haki ipatikane.

Aidha Aveva aliwataja waandishi wa habari kuwa wamekuwa chanzo cha migogoro ndani ya Simba kutokana na kuripoti vibaya habari za klabu yake na kuwachochea mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.

"Waandishi mmekuwa sehemu ya migogoro ndani ya Simba na kuna redio moja hapa mjini ndiyo inasababisha kwa kuwapigia watu wa nje kuzungumzia mambo muhimu ndani ya klabu" alisema Aveva.

Pia Aveva amewataja wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuwa wamechangia kwa kiasi kikubwa kutochukua ubingwa kutokana na kutokuwa wavumilivu mpaka ikafika hatua wanalipiga mawe basi la timu na kumjeruhi mchezaji wetu.

"Katika mpira kuna matokeo matatu na wanajua lakini walitugeuka na kututukana kuwapiga viongozi na basi la Wachezaji sasa kwa mazingira hayo ubingwa utaupataje" alihoji Aveva .

Post a Comment

 
Top