BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
SIKU moja baada ya Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) kuipokonya pointi tatu timu ya Azam kwa kosa la  kumchezesha beki wao Erasto Nyoni aliyekuwa na kadi tatu za njano, Uongozi wa timu hiyo umelijia juu shirikisho hilo na kusema linaongozwa kwa majungu.

Azam ilimchezesha Nyoni katika mchezo namba 156 dhidi ya Mbeya city uliochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kukiuka kanuni ya 37(4) ya ligi kuu toleo la mwaka 2015 na kanuni ya 14(37) ya mwaka jana.

Mtendaji Mkuu wa timu hiyo Saady Kawemba ameiambia BOIPLUS kuwa: ''Kwa uongozi huu wa shirikisho hilo tutaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu kwa kuwa kuna maamuzi yanafanywa ili kuwapa faida timu fulani. Tuliisajili Azam kama timu ya mpira hivyo tutaendelea kucheza ila utaratibu unaofanywa na TFF ndiyo unaodumaza soka na tumefunga mjadala sasa tunaangalia fainali za Kombe la FA,''

Azam imeshuka hadi nafasi ya tatu baada ya kubakiwa na alama 57 wakiwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya Simba ambao wana mchezo mmoja mkononi huku Yanga ikiendelea kubaki kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 68.

Azam watashuka dimbani kesho Jumamosi kuwakabili Kagera Sugar mechi itakayochezwa Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga huku wenyeji wakihitaji pointi tatu ili kujinusuru kushuka daraja.

Post a Comment

 
Top