BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
 PRISONS imeamua kuikamia Coastal Union ambao wameshuka daraja kwani leo hii wamefanya mazoezi yao mchana wa jua kali, sababu kubwa ni kutaka kuzoea hali ya hewa ya joto kama ilivyo jijini Tanga ambako watacheza mechi hiyo ya mwisho, Mei 22, Jumapili.

Kocha wa Prisons, Salum Mayanga amekusudia kumaliza ligi akiwa ameshinda mechi yake ya mwisho ili ashike nafasi ya nne wakifuta ndoto za Mtibwa Sugar ambao wapo nafasi ya tano baada ya kupoteza mechi yao iliyopita dhidi ya Simba.

Mayanga aliwapeleka wachezaji wake kwenye mazoezi mchana wa saa saba ambapo aliwapigisha kwata kwa muda wa saa moja ambapo kipa wa timu hiyo Beno Kakolanya ambaye ameitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza, alisema kuwa mazoezi hayo yatawafanya wamudu hali ya hewa ya jiji la Tanga.

"Kwanza nashukuru kuitwa kwenye kikosi cha Stars, niliamini ipo siku nitaitwa kikubwa ni kuongeza juhudi pamoja na kujituma, tumefanya mazoezi mchana huu kwasababu ya kuzoea hali ya hewa ya Tanga, Tanga kuna joto na mara kadhaa huwa linatusumbua tukienda kucheza na timu za huko.

"Coastal wameshuka daraja lakini hatuwadharau, ni timu bora na tunataka kushinda mechi hiyo ili kuendelea ushindi na lengo letu ni kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, lengo hilo tuliliweka tangu awali kuwa tumalize ligi tukiwa kwenye nafasi hiyo," alisema Kakolanya

Prisons imekusanya pointi 48 ambapo Mtibwa Sugar wenyewe wana pointi 47 huku kila mmoja akimwombea mwenzake apoteze mechi ya mwisho ili aweze kujinyakulia kitita cha Sh 23 milioni.

Yanga ambao ni mabingwa wa VPL watajinyakulia Sh 81 milioni, mshindi wa pili atapataSh 40 milioni ambapo atakuwa kati ya Simba au Azam huku mshindi wa tatu atapewa Sh 29 milioni.

Post a Comment

 
Top