BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
BAADA ya kusuasua kwa zoezi la uchuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya Klabu ya Yanga, Baraza la Michezo Tanzania (BMT) limeagiza uchaguzi huo ufanyike katika tarehe iliyopangwa ya Juni 15.

Baraza hilo liliitaka klabu hiyo kufanya uchaguzi mkuu mwezi ujao baada ya kuongeza muda kwa viongozi walio madarakani wa mwaka mmoja na nusu ambao ni kinyume cha katiba lakini kwa hali ilivyo inaonekana utanaendelea kupigwa danadana baada ya wanachama wake kugoma kuchukua fomu za kugombea.

Kaimu Katibu mkuu wa Baraza hilo Mohammed Kiganja alisema kuna vikao vinavyoendelea kutoka kwa wanachama wa klabu hiyo na baadhi ya wajumbe wa TFF kwa ajili ya kuhujumu uchaguzi huo usifanyike kwa maslahi yao binafsi.

Kiganja aliyazungumza hayo mbele ya waandishi wa Habari katika ofisi za BMT na kusema kuwa endapo kuna mtu atabainika kuhujumu zoezi hilo atachukuliwa hatua za kisheria kwakuwa utaratibu ulitolewa juu ya zoezi zima la uchaguzi.

"Uchaguzi upo pale pale na utaratibu wote ulishatolewa kilichobaki ni utekelezaji tu na hakuna kitakachobadilika," alisema Kiganja

Katibu mkuu wa klabu hiyo Deusdedit Baraka alipotafutwa kutoa maelezo kuhusu tamko hilo la BMT simu yake iliita bila kupokelewa.

Uchaguzi huo kwa mujibu wa Katiba ya Yanga ulikuwa ufanyike mwezi wa 12 mwaka 2015.

Post a Comment

 
Top