BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Shinyanga
WACHEZAJI Haruna Chanongo, Rajabu Zahir na Abuu Ubwa wa Stand United ni kama wametimuliwa kikosini baada ya kocha wao Patrick Liewig kuwapa likizo ya mwezi mmoja na kuwoandoa kwenye mipango yake katika mechi zilizobaki.

Tayari uongozi wa Stand umewaandikia barua wachezaji hao ingawa bado hawajapewa na imeelezwa kuwa watapewa barua zao muda wowote kwani hata mazoezini wamezuiliwa.

BOIPLUS inafahamu kwamba mikataba ya wachezaji hao inamalizika mwishoni mwa msimu ambapo wachezaji hao pia ndiyo utakuwa mwisho wa mapumziko yao waliyopewa na Liewig.

Sababu kubwa ya kupumzishwa na kuondolewa kwenye mipango ni kudaiwa kucheza chini ya kiwango na kupelekea timu yao kupata matokeo mabaya ingawa wachezaji hao waliingia kwenye mgogoro na kocha wao mapema mwaka huu.

Liewig alikiri juu ya hilo na kwamba anasubiri kuwapa barua zao muda wowote kuanzia sasa akisisitiza kutofurahishwa na tabia za wachezaji hao.

BOIPLUS iliwatafuta wachezaji hao ambao walikiri kutoruhusiwa kufanya mazoezi ya timu tangu walipocheza mechi yao na Mwadui ambayo walipoteza kwa bao 2-1. 

''Tulipata taarifa kutoka kwa kocha msaidizi Athuman Bilali kuwa kocha amesema tusiende mazoezi, hivyo tupo tunawasubiri wao, tulipoteza mechi hiyo kwa makosa ya uwanjani na si vinginevyo,'' alisema. 

Mratibu wa timu hiyo Mbasha Matutu alisema kuwa wachezaji hao wataendelea kulipwa mishahara yao kama kawaida mpaka mikataba yao itakapomalizika.

''Kocha amewaondoa wachezaji hao kwasababu hawapo kwenye programu yake hivyo amewapa likizo ya mwezi mmoja kuanzia Mei Mosi ila haki zao zote watazipata kulingana na mikataba yao, bado hatujawapa barua ila watapewa muda wowote tu na wameambiwa tayari,'' alisema Mbasha.

Post a Comment

 
Top