BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar
WAKATI timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ikielekea nchini Kenya kumenyana na Harambee Stars katika mchezo wa kirafiki, nahodha wa timu hiyo Mbwana Samatta bado yupo Ubelgiji akiitumikia KRC Genk.

Samatta ameshindwa kujiunga na Stars kwa wakati kutokana na kubanwa na majukumu ya klabu yake ambayo inagombea nafasi ya kushiriki michuano ya Europa 2016/17.

"Nimeshindwa kuwahi, tunapambana kufuzu Europa kwahiyo si rahisi kuruhusiwa kuondoka hapa, ni hadi tumalize mchezo wa marudiano," alisema Samatta katika mahojiano na BOIPLUS.

Genk imepangwa kucheza na Charleroi katika mtindo wa mtoano ili kufuzu michuano hiyo ambapo katika mchezo wa jana, Genk ilipigwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa ugenini, Stade du Pays de Charleroi na sasa wanahitajika kushinda kuanzia mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano ili wafuzu.

Mechi hiyo itachezwa Jumapili Mei 29 katika uwanja wa nyumbani wa Genk, Cristal Arena na baada ya hapo Samatta ataanza safari ya kuja kujiunga na Stars.

Stars inajiandaa kuvaana na Misri katika michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika.

Post a Comment

 
Top